Comoro yajitayarisha kwa uchaguzi wa rais
11 Januari 2024Assoumani, ambaye alikuwa mwenyekiti wa kupokezana wa Umoja wa Afrika mnamo mwaka uliopita anachuana na wanasiasa wengine watano. Wanasiasa wengine wa upinzani wametoa wito wa kususiwa uchaguzi huo wakiituhumu tume ya uchaguzi kukipendelea chama tawala, madai ambayo tume hiyo imekanusha.
Wakati wa uchaguzi uliopita wa mwaka 2019 waangalizi wa kikanda walisema kulikuwa na dosari nyingi na matokeo ya kura hiyo yalipungikiwa uhalali.
Uchaguzi huo ambao uliitishwa mapema ulifuatiwa na mabadiliko ya katiba yaliyoondoa sharti la nafasi ya urais kuwa ya kupokezana miongoni mwa visiwa vitatu vikubwa vinavyounda Jamhuri ya Comoro.
Mabadiliko hayo ndiyo yanamwezesha rais Assoumani kuwania muhula mwingine madarakani. Assoumani, ambaye ni afisa wa zamani wa jeshi anakosolewa kwa kuongoza taifa hilo la visiwa vya bahari ya Hindi kwa mkono wa chuma na kukandamiza wakosoaji wote wa utawala wake.