Condolezza Rice asema amani kati ya Israel na Palestina inawezekana mwaka huu
4 Machi 2008Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condolezzar Rice amesisitiza juu ya matumaini yake kwamba mpango wa amani kati ya wapalestina na waisrael ulioanzishwa na rais Bush mwezi Novemba mwaka jana mjini Annapolis Marekani utafanikiwa.
Condolezza Rice amelishutumu kundi la Hamas linalodhibiti Ukanda wa Gaza juu ya mapambano mapya ambayo yalizuka hivi karibuni katika eneo hilo la mashariki ya kati.Isreal imeondoa wanajeshi wake katika Gaza lakini imeapa kuendelea na mashambulio dhidi ya wanamgambo wa eneo hilo wanaodaiwa kufyatua roketi ndani ya miji ya Israel.Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani amesema mazungumzo yaliyoanzishwa na rais Bush yanaweza kufanikiwa kufikia mwishoni mwa mwaka huu.Hata hivyo bibi Rice ameshindwa kukosoa hatua ya Israel ya kuendesha mashambulio ya angani dhidi ya Gaza ambayo yamesababisha kuwawa kwa wapalestina kadhaa katika kipindi cha siku mbili zilizopita wakiwemo wanawake na watoto badala yake amesema ni hatua iliyochukuliwa na taifa hilo kwa lengo la kujilinda.Bibi Rice ambaye yuko Misri katika ziara ya muda mfupi mashariki ya kati amezitaka Israel na Palestina kurudi kwenye meza ya mazungumzo mara moja.Rais Mahmoud Abbas alisimamisha mawasiliano na Israel wiki hii baada ya taifa hilo kunzisha opresheni hiyo ya kijeshi dhidi ya watu wa Gaza.