1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Confederations Cup ; Brazil yaibuka kidedea

1 Julai 2013

Pazia lashuka katika michuano ya kombe la mabara nchini Brazil, mabingwa wa Ulaya na dunia Uhispania waonja " joto ya jiwe" , Brazil yaibuka kidedea.

From L to R) Brazil's Fred celebrates with teammates Neymar, Paulinho and Oscar after scoring against Spain during their Confederations Cup final soccer match at the Estadio Maracana in Rio de Janeiro June 30, 2013. REUTERS/Jorge Silva (BRAZIL - Tags: SPORT SOCCER TPX IMAGES OF THE DAY) / Eingestellt von wa
Brazil wakishangiria baoPicha: Reuters

Je kipigo cha jana(30.06.2013) cha mabao 3-0 ilichokumbana nacho mabingwa wa dunia na Ulaya Uhispania dhidi ya Brazil katika fainali ya kombe la mabara, Confederations Cup , ni kwikwi tu ama inatoa ishara ya mwisho wa enzi za tiki taka ya kikosi hicho cha La Roja?.

Hilo ndio swali ambalo vyombo vya habari vya Uhispania na wadadisi wengine wa masuala ya soka duniani walikuwa wanajiuliza leo, baada ya kipigo cha kudhalilisha katika mchezo wa kwanza wa mashindano kwa Uhispania tangu mwaka 2010.

Kocha wa Uhispania Vicente del BosquePicha: AP

Vyombo vingi vya habari za michezo vimejaribu kuangalia kadhia hiyo iliyowapata Uhispani kuwa ni bahati mbaya tu katika siku mbaya kwa kocha Vicente del Bosque na kikosi chake.

Kwa mfano kichwa cha habari katika gazeti maarufu la Marca kinasema , "Tutarejea", wakiashiria fainali za kombe la dunia mwakani nchini Brazil.

Del Bosque akiri

Del Bosque binafsi ameweka msisitizo katika matamshi kama hayo kwa kusema , "mara nyingine ni vizuri kushindwa, tumekuwa hatuna bahati kwa kufungwa mabao katika wakati muhimu. Goli la kwanza lilikuwa muhimu lakini hiyo haiwezi kuwa sababu iliyosababisha tufungwe.

Walicheza mchezo wa kuweka mbinyo dhidi ya timu yetu na kuvunja mtiririko wa mchezo wetu kwa kufanya rafu nyingi. Hata hivyo kocha huyo mzoefu , ambaye ameiongoza uhispania kupata ushindi katika kombe la dunia mwaka 2010 na Euro 2012, alikuwa mwepesi pia kuwapongeza Brazil. ilikuwa timu nzuri sana dhidi yetu ni mabingwa wanaostahili. Amesema Del Bosque.

Brazil inashauku kubwa wakati inajiwinda kuingia katika fainali za kombe la dunia mwaka 2014 nchini humo kwa mtazamo tofauti baada ya pazia kushuka katika kinyang'anyiro cha kombe la mabara jana.

Confederations Cup imeelezwa na rais wa shirikisho la kandanda duniani FIFA Joseph Sepp Blatter kuwa ilikuwa ni tamasha murua kabisa.

Maandamano nchini BrazilPicha: LLUIS GENE/AFP/Getty Images

Maandamano

Hata hivyo mashindano hayo yaliyojumuisha timu nane yaliyofanyika katika viwanja sita kati ya 12 ambavyo vitatumika kwa fainali za kombe la dunia yamefanyika huku kukiwa na maandamano tangu mwanzo hadi siku ya mwisho nchi nzima.

Polisi wakuzuwia ghasia walitanda , na ghasia ziliendelea mjini Rio de Janeiro karibu na uwanja uliofanyika fainali hiyo wa Maracana.

Rais wa FIFA Joseph BlatterPicha: dapd

Neymar nyota inayong'ara

Lakini nyota anayechipukia wa Brazil Neymar alijitokeza kuwa mmoja wa vijana watakaoweza kuichukua Brazil katika kiwango cha juu katika medani ya soka ya dunia. Alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa michuano hiyo, alipachika wavuni mabao manne na kutoa pasi kadha za kufunga mabao kwa wenzake, na huenda muhimu zaidi amekuwa kiongozi muhimu katika kikosi cha timu ya Brazil cha 'Verdeamarela'.

Nyota wa Brazil Neymar da Silva Santos JuniorPicha: Reuters

Wachezaji wa Uhispania pia walifurahishwa na mchezaji huyo, kama anavyosema mlinzi wa Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania Gerard Pique ambaye alitolewa kwa kadi nyekundu zikiwa zimesalia dakika 20 kabla ya mchezo wa fainali kumalizika , kwa kumwangusha Neymar ambaye atakuwa mchezaji wa timu yake ya Barcelona , karibu na eneo la hatari.

"Ni hodari sana. Ni mchezaji mwenye kipaji cha hali ya juu kabisa, ni mwepesi wa kwenda kasi , ameonesha hali hiyo muda wote wa mashindano. Na zaidi ya hayo anafunga magoli. ninafurahi sana kwa kuwa atakuwa upande wetu mwaka ujao na Barcelona."

naye mwenyewe Neymar kuhusu ushindi wa Brazil amesema ulikuwa muhimu sana.

"Leo ndoto yangu imekuwa kweli. Nina furaha sana. Na ulikuwa mchezo mzuri na tumenyakua taji hili."

Mshambuliaji wa Brazil Fred ambaye alipachika mabao mawili usiku wa jana aliuelezea ushindi huo kuwa ni mtamu sana kwao.

"Ulikuwa ni ushindi mnono , ukitilia maanani hisia za pamoja za wachezaji wetu na kazi tuliyokuwa tukiifanya kwa muda mrefu pamoja na kocha Felipe Scolari. Katika wakati fulani , kulikuwa na ukosefu wa kujiamini baina ya wachezaji na wafanyakazi wa timu na ukosefu wa kujiamini kwa nje, lakini tumeweza kuwavuta mashabiki upande wetu."

Mlinda mlango wa Italia hata hivyo naye alikuwa shujaa jana baada ya Italia kuichapa Uruguay kwa mikwaju ya penalti na kujipatia nafasi ya tatu katika kombe la mabara. Gianluigi Buffon , bingwa wa dunia mwaka 2006 ambaye alikuwa anacheza mchezo wake wa 133 na kikosi cha Azzurri , Italia, alizuwia mikwaju wa penalti mitatu katika mchezo huo ambao ulikuwa sare kwa mabao 2-2 hadi dakika 120 za mchezo huo.

Mlinda malango wa Italia Gianluigi BuffonPicha: Getty Images

Ethiopia yaadhibiwa

Kwa upande wa Afrika , Afrika kusini imepata kamba ya kuiokoa katika kuwania kufuzu katika fainali za kombe la dunia mwakani baada ya Ethiopia kunyang'anywa points tatu muhimu na shirikisho la kandanda duniani FIFA kwa kumchezesha mchezaji ambaye hakustahili kucheza katika mchezo dhidi ya Botswana .

Katika taarifa iliyotolewa na FIFA , imesema Minyahile Teshome Beyene hakupaswa kucheza katika mchezo huo kwa kuwa alikuwa na kadi za njano zinazomzuwia kushiriki mchezo huo ambao Ethiopia iliishinda Botswana mabao 2-1.

Ushindi kwa hiyo umekwenda kwa Botswana kwa mabao 3-0 na Ethiopia ambayo ilikuwa ikiongoza kundi A kwa zaidi ya points tano imerudishwa nyuma na sasa inaongoza kwa points mbili tu. Ethiopia bado wana nafasi ya kufuzu wakati watakapotembelea jamhuri ya Afrika ya kati katika mchezo wao wa mwisho hapo Septemba 6, wakati Afrika kusini itaikaribisha nyumbani Botswana.

Leo (01.07.2013) , umefunguliwa rasmi msimu wa wachezaji kuhama, ambapo mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Uturuki Halil Altintop anarejea katika Bundesliga akijiunga na Augsburg kwa mkataba wa miaka miwili. Mshambuliaji wa Uhispania Fernando Llorente anatarajiwa kuwasili mjini Turin kujiunga na timu yake mpya ya Juventus Turin na atafanyiwa uchunguzi wa afya.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / dpae / ape

Mhariri:Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi