1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Congo ipo njia panda ikisubiri matokeo ya uchaguzi

5 Januari 2019

Wasiwasi umetanda mjini Kinshasha wakati watu wakisubiri kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi. Baadhi ya wananchi wanahofia kuzuka ghasia katika nchi hiyo anasema mwandishi wa DW Jonas Gerding.

Demokratischen Republik Kongo | Wahlkommision |  Wahlautomat
Picha: DW/F. Quenum

Tarehe iliyopangwa na tume ya uchaguzi ya kutangaza matokeo hayo siyo jambo la pekee ambalo ni muhimu. Hayo amesema Patrick Kanyinda mwanafunzi anayesomea taaluma ya uhandisi wa ujenzi kwenye chuo kikuu cha Kinshasa chenye wanafunzi wapatao 20,000. Kanyinda amesema ikiwa kura za wanachi zitaibwa, wanafunzi  watakuwa wa kwanza kujitokeza barabarani ili kupinga.

Amesema hilo ni jambo la uhakika. Kanyinda ameeleza kuwa hawatasubiri maagizo ya wengine.  Kijana huyo ni mmojawapo wa  wanaharakati, na yeye ndiye anayeratibu shughuli za jumuiya mojawapo ya vijana wa nchini Kongo inayoitwa Lucov.

Vijana hao hivi karibuni walifanya maandamano makubwa ya kumtaka rais Joseph Kabila asigombee  muhula mwingine na pia kutaka uchaguzi ufanyike kwa haki. Vijana hao wako tayari kuchukua hatua, hata ikiwa mbele ya risasi na gesi ya kutoa machozi kama ilivyotokea mnamo siku za nyuma.

Kanyinda amesema kwamba hawaogopi chochote, amesema hawapogi kufa wala kupelekwa jela. Mratibu huyo wa jumuiya ya Lucov amesema ikiwa safari hii tena mabadiliko ya uongozi yatadhulumiwa, kisu  kitakuwa kimefika mfupani! 

Mwanaharakati huyo kijana ameeleza kuwa vijana watajitokeza barabarani kwa fuhara kubwa ikiwa mgombea mmojawapo wa upinzani atashinda uchaguzi. Mwanafunzi huyo amesema watasherehekea ushindi ikiwa kura za wananchi zitaheshimiwa.

Rais wa tume huru ya uchaguzi nchini Congo Corneille Nangaa YobeluoPicha: Getty Images/AFP/L. Tato

Kwa mara ya kwanza katika historia yake huenda Jamhuri  ya Kidemokrasia ya Congo ikashuhudia mabadiliko ya uongozi kwa njia ya kidemokasia. Ni kwa kiasi gani mabadiliko hayo yatatekelezwa kwa amani itaonekana hapo baadae baada ya jina la mshindi litakapotangazwa. Iwapo makabidhiano hayo yatakuwa ya amani bado linabaki kuwa swali ambalo linasubiri jibu. Mwanafunzi huyo wa chuo kikuu na mratibu wa kundi la Lucov amesema kwa sasa huwezi kutofautisha matukio yajayo kama kutakuwa na vurugu mabarabarani au kutakuwa na furaha, nderemo na vifijo?

Wakati huo huo kanisa katoliki lenye ushawishi mkubwa nchini Kongo limesema yuko mshindi wa wazi wa  uchaguzi uliofanyika Jumapili iliyopita kulingana na matokeo iliyoyaona. Maaskofu wa kanisa hilo wamewataka wahusika wawe wakweli na watangaze matokeo haraka.

Kanisa hilo liliwaweka maelfu ya waangalizi wake na baadhi yao wanatoa taarifa juu ya kutokea hitilafu. Lakini tume ya uchaguzi imesema tangazo la matokeo lilonatarajiwa kutolewa hapo kesho linaweza kuahirishwa. Mkuu wa tume hiyo Corneille Nangaa amesema tume yake bado inasubiri vituo vya kupigia kura vipeleke  zaidi ya asilimia 80  ya hesabu za kura.

Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika zinaishinikiza serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, zikiitaka iheshimu uamuzi wa wapiga kura huku muda wa mwisho kabla ya kutangazwa matokeo ukikaribia. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana siku ya Ijumaa kujadili uchaguzi wa Congo lakini halikutoa taarifa yoyote ila litakutana tena siku ya Jumanne ijayo.

Mnamo siku ya Alhamisi Wizara ya Mambo ya Nchi ya nje ya Marekani ilitoa wito kwa Tume Huru ya Uchaguzi nchini Congo CENI kuhakikisha kuwa kura zinahesabiwa kwa umakini, Marekani imetishia kuwawekea vikwazo watakaohujumu mchakato huo au kutishia amani na utulivu wa nchini Congo.

Mwandishi: Zainab Aziz/Gerding, Jonas (HA Afrika)/ http://www.dw.com/a-46962073/AFP

Mhariri: Buwayhid, Yusra

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW