1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Congo kuanzisha mfuko maalum kusimamia misaada ya kiutu

Sylvia Mwehozi
18 Aprili 2018

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inapanga kuanzisha mfuko maalumu wa kusimamia misaada yote chini ya rasimu mpya ya sheria, wiki moja baada ya kushindwa kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa wafadhili mjini Geneva Uswisi. 

Ruanda Kiziba Flüchtlingslager
Picha: Reuters/J. Bizimana

Umoja wa Mataifa unatafuta kiasi cha dola bilioni 2.2 ili kuwasadia watu milioni 13 nchini Congo kwa mwaka huu waliokumbwa na migogoro ya kibinadamu inayosababishwa na migogoro ya kikabila na wanamgambo na kurejesha kumbukumbu mbaya ya vita ya wenyewe kwa wenyewe ya mwaka 1998-2003.

Katika mkutano wa wafadhili wiki iliyopita, wafadhili wa kimataifa waliahidi dola milioni 528 kuelekea juhudi hizo, ikiwemo kuwapatia chakula watoto milioni 2.2 wanaokabiliwa na utapiamlo mkali na kuwafanya kuwa katika hatari ya kifo kutokana na maradhi hayo.

Kwenye taarifa yake baraza la mawaziri la Congo limesema kwamba shirika jipya la mfuko wa usimamizi wa misaada ya kibinadamu, litakuwa na jukumu la kusimamia, kufuatilia na kudhibiti misaada ya kiutu na kufanyia kazi njia zote za  mtiririko wa fedha unaoathiri sekta ya kibinadamu katika nchi.

Sehemu ya wajumbe waliohudhuria mkutano wa kuisadia CongoPicha: picture-alliance/dpa/BELGA/E. Lalmand

Haikuwa wazi ni namna gani mfuko huo utafanya kazi, ikiwa wafadhili wa kimataifa watakubali kutuma fedha kwenye akaunti inayoendeshwa na serikali ya Kinshasa na ikiwa mfuko huo mpya utahatarisha fedha zilizokwisha kubaliwa chini ya sheria za nyuma.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema wanasubiri ufafanuzi wa kina kutoka serikali ya Congo kabla ya kutoa kauli juu ya hilo. Hata hivyo, uamuzi wa kubadili namna inavyopokea ufadhili, umekuja wakati sio mzuri kwa taifa hilo la afrika ya kati mzalishaji wa shaba.

Uamuzi wa rais Joseph Kabila kukataa kuondoka madarakani wakati muhula wake ulipomalizika mwaka 2016, umesababisha kuvunjika kwa mamlaka hususan maeneo mengi ya ndani ya mashariki mwa Congo, na kuongeza umri katika mgogoro wa zamani uliochangia watu milioni 4.3 kuyakimbia makazi yao.

Uamuzi huo pia unakwenda sambamba na kudhoofika kwa mahusiano ya Congo na jumuiya ya kimataifa uliochangiwa na uamuzi wa Kabila wa kukataa kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa wa wafadhili uliofanyika mjini Geneva wiki iliyopita.

Kinshasa imekataa kuwepo na mgogoro wa kibinadamu katika taifa hilo kubwa la Afrika ya Kati na kuyatuhumu mataifa ya kigeni kwa kuishutumu nchi hiyo na kuharibu uwekezaji.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW