Congo kuzinduwa sensa ya watu na vitambulisho vya uraia
17 Septemba 2021Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetoa wito kwa raia wa nchi hiyo kujitayarisha kushiriki sensa ya watu itakayotumika pia kutoa vitambulisho vya uraia kwa Wakongomani. Hata hivyo baadhi ya wanasiasa nchini Kongo wanahofia kuwa zoezi la kuhesabu watu huenda litatumika kama kisingizo cha kuchelewesha uchaguzi mkuu unaopangwa kufanyika mwaka 2023. Jean Noël Ba-Mweze anaripoti kutoka Kinshasa.
Serikali ya Congo imesema itafanya sensa ya watu hivi karibuni ikiwa imepita miaka 37 tangu zoezi la kuhesabu watu lilipofanyika kwa mara ya mwisho nchini humo.Ni mwaka 1984 wakati Congo ilipokuwa chini ya utawala wake Marshal Joseph-Desiré Mobutu ndiyo sensa ya mwisho ilifanyika.
Kutambua idadi rasmi ya wakaazi wa Congo
Mbali ya kutofanyika sensa kwa muda mrefu, wakongomani hawana pia vitambulisho vya uraia.
Rais Félix Tshisekedi alipoingia madarakani Januari 2019,aliahidi kutatua suala hilo na hivi sasa, tume toka wizara tofauti imeandaa mwongozo wa kuendesha zoezi la kuwatambua watu kupitia sensa pamoja na uandikishaji wa wapiga kura.
Operesheni ya kutambua idadi ya wakaazi wa Kongo itazinduliwa hivi karibuni, kama alivyoeleza Daniel Aselo, Naibu Waziri Mkuu anayehusika na mambo ya ndani.
''Kazi hizo za tume zilifikiria kuandaa namna ya kufanya zoezo la utambuzi wa idadi ya watu ambayo itatangazwa hivi karibuni. Kwa hivyo, serikali itashughulikia kifedha na kiufundi, wakati wa operesheni za kutambua idadi ya watu.'', alisema Aselo.
Soma pia :zawadi ya rais Tshisekedi kwa wabunge yazuwa gumzo
Wasiwasi wa upinzani
Swali hilo linaendelea kuwagawanya wanasiasa. Wapinzani wa Rais Tshisekedi wanamshukia kutumia sensa ya raia ili kujaribu kuchelewesha uchaguzi unaotarajiwa hapa nyumbani mwaka 2023.
Prince Epenge ni Kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ya Kongo (ADDC), pia ni msemaji wa muungano wa upinzani Lamuka.
''Tangazo la Waziri wa Mambo ya Ndani linaleta hofu ya watu kuona kwamba Felix Tshisekedi anajiongezea muda madarakani. Sisi na raia tutapinga. Watu wanataka serikali iandae operesheni ya kuwatambua na kuwahesabu wapiga kura. Ulimwengu mzima umeelewa kuwa Felix hataki uchaguzi.'', alisema Epenge.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilikuwa na wakaazi milioni 29.9 baada ya sensa ya mwisho mwaka 1984. Hivi leo nchi hii inakadiriwa kuwa angalau wakaazi milioni mia moja , ila kwa kweli idadi kamili haijajulikana baada ya kupita miaka mingi bila raia kuhesabiwa.