1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Congo na Guinea ya Ikweta zatinga nusu fainali

1 Februari 2015

Soka barani Afrika limepata kufikia hali ya juu ya kupendeza lakini pia liliingia doa Jumamosi (31.01.15), kutokana na vitendo vya fujo pale mwamuzi aliposhambuliwa baada ya wenyeji Guinea ya Ikweta kuishangaza Tunisia.

Afrika Cup 2015 Kongo
Mashabiki wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo wakishangiria ushindiPicha: AFP/Getty Images/C. de Souza

Guinea ya Ikweta imeishangaza Tunisia kwa kuitoa nje ya mashindano ya kombe la mataifa ya Afrika katika robo fainali.

Pambano la kwanza la kufurahisha baina ya Congo mbili, Congo Brazzaville na Congo Kinshasa, pambano ambalo lilishuhudia mabao sita yakitinga wavuni katika uwanja wa Estadio de Bata, lilionesha matumaini makubwa jioni hiyo, lakini vituko ndani ya uwanja katika pambano la pili la robo fainali lilichafuliwa na matukio ya kuchukiza wakati refa aliporushiwa makonde na kupigwa mateke na wachezaji wenye hasira wa Tunisia.

Mpambano uliogubikwa na hasira na fujo kati ya Guinea ya Ikweta na TunisiaPicha: AFP/Getty Images/K. Desoukia

Walikuwa wamejawa hasira kwa kile kinachoonekana kuwa ni kushindwa kwa refa kutenda haki baada ya Guinea ya Ikweta , moja kati ya nchi ndogo kabisa katika bara la Afrika na wenyeji waliochukua jukumu hilo kwa dharura, wakitoa mshituko mkubwa kabisa katika historia ya fainali hizi za kombe la Afrika kwa kupata ushindi wa mabao 2-1 baada ya pambano lao kuingia katika dakika za nyongeza.

Wameingia katika awamu ya timu nne pamoja na jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, ambao walikuwa nyuma kwa mabao 2 lakini waliweza kuwaangusha majirani zao wa kaskazini Congo Brazzaville kwa mabao 4-2 katika pambano la kwanza la kuvutia la robo fainali.

Wachezaji wa Congo Brazzaville na Congo Kinshasa wakipambanaPicha: AFP/Getty Images/K. Desoukia

Lakini ushindi wa Guinea ya Ikweta uligubikwa na aina ya ushindi wao pamoja na hatua ya ghasia iliyooneshwa na wachezaji wa Tunisia, ambao walikuwa wanapigiwa upatu kutoroka na taji hilo dhidi ya kikosi cha wachezaji ambao wengi wao wanacheza soka katika madaraja ya chini nchini Uhispania na kuonekana wakiwa njiani kuelekea katika nusu fainali wakati walipopata bao la kuongoza katika dakika ya 70.

Lakini goli la Ahmed Akaichi lilifutwa katika dakiika za majeruhi wakati wenyeji wa mashindano hayo walipopewa mkwaju wa penalti na refa kutoka Mauritius Seechurn Rajindraparsad, ambayo iliwekwa wavuni na Javier Balboa.

Penalti hiyo ilikuwa mwishoni mwa pambano hilo lililokuwa na mvutano na kutumbukia zaidi katika vurugu wakati wachezaji wa akiba wa timu zote walipoanza kurushiana chupa za maji na kutukanana kabla ya kuanza kukabana mwishoni mwa mchezo huo.

Wachezaji wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo wakipongezana baada ya ushindi dhidi ya CongoPicha: AFP/Getty Images/K. Desouki

Katika wakati huo Guinea ya Ikweta ilikuwa tayari imechukua uongozi wa pambano hilo kwa ushindi wa mabao 2-1 baada ya mkwaju wa Balboa katika dakika ya 102, mchezaji wa zamani wa timu ya vijana ya Real Madrid.

Mapambano nje ya uwanja yalifuatiwa na pia na mikwara ya hapa na pale ndani ya uwanja na baada ya firimbi ya mwisho kupulizwa , refa aliondolewa haraka na polisi kutoka uwanjani, lakini si kabla ya kupelekwa mbio na wachezaji wa Tunisia ambao walimpiga mateke na kupiga makonde.

Adhabu huenda ikafuata.

Mchezo huo umetofautiana sana na mapambano la kuvutia la ufunguzi wa michuano hiyo ya robo fainali wakati Dieumerci Mbokani alipopachika mabao mawili na kuongoza kikosi hicho cha chui wa Congo kutoka nyuma na kupata ushindi dhidi ya Congo Brazzaville.

Kikosi cha timu ya taifa ya GuineaPicha: KHALED DESOUKI/AFP/Getty Images

Ferebory Dore alifungua ukurasa wa mabao jioni ya jana akipachika bao katika dakika ya 55 na Thievy Bifouma alipachika bao la pili dakika saba baadaye lakini jamhuri ya kidemokrasi ya Congo ilirejesha mabao hayo, wakipachika mabao manne katika dakika 25 za kipindi cha pili.

Mbokani alifungua kitabu cha Chui hao na kukifunga, ambapo Jeremy Bokila na Joel Kimwaki wakiongeza bao la pili na la tatu na kuipeleka Congo DRC katika nusu fainali tangu mwaka 1998.

Watakutana na ama Cote D'Ivoire ama Algeria mjini Bata siku ya Jumatano katika nusu fainali.

Guinea ya Ikweta itacheza mjini Malabo siku ya Alhamis dhidi ya amani Ghana ama Guinea.

Kikosi cha Tembo wa Cote D'IvoirePicha: I. Sanogo/AFP/Getty Images

Nafasi ya Algeria , kama timu iliyoko nafasi ya juu katika bara la Afrika iko mashakani leo wakati inakabiliana na timu kamambe ya Cote D'Ivoire katika mchezo wa mwisho wa robo fainali katika kombe la mataifa ya Afrika.

Mpambano huo kati ya vigogo viwili unatanguliwa katika uwanja wa Nuevo Estadio de Malabo na mchezo kati ya Ghana na Guinea, timu ambayo njia yake kuingia katika kinyang'anyiro hiki cha timu nane ilipatikana baada ya kura baada ya kufungana na Mali kwa pointi, magoli ya kufunga na kufungwa.

Guinea ambayo ilivuka vikwazo kadhaa baada ya kuzuka ugonjwa wa Ebola nchini humo na kufikia hadi ilipo hivi sasa , inakabiliwa na kikwazo kingine Ghana, ambayo iliweza kuonesha umahiri mkubwa baada ya kupambana kiume kutoka nyuma katika duru ya kwanza na kupata nafasi ya kwanza katika kundi lao.

Kikosi cha timu ya taifa ya AlgeriaPicha: K. Kudryavtseva/AFP/Getty Images

Cote D'Ivoire itapata huduma ya mshambuliaji Gervinho ambaye anarejea uwanjani baada ya kutumikia adhabu na kuimarisha kikosi hicho ambacho tayari kinaonekana kuwa na nyota wengi dhidi ya Algeria, mbele ya timu iliyo katika nafasi ya 18 ya timu za Afrika katika orodha ya shirikisho la kandanda duniani FIFA.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Sudi Mnette

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW