Congo na Rwanda zapiga hatua katika mchakato wa amani
26 Novemba 2024Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda zimesaini waraka muhimu kuimarisha mchakato wa kutafuta amani katika eneo linalokabiliwa na machafuko la mashariki mwa Congo. Hayo yamesemwa jana Jumatatu na Angola ambayo inasimamia mchakato huo.
Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Angola imesema mawaziri wa mambo ya nje wa Congo na Rwanda waliridhia waraka wa dhana ya uendeshaji, chombo muhimu kinachopaswa kuweka masharti ambayo kwayo wanajeshi wa Rwanda wataondoka kutoka ardhi ya Congo.
Hata hivyo taarifa hiyo ya serikali ya Angola haikutoa taarifa zozote kuhusiana na taratibu zitakazopitishwa.
Rasimu ya awali ya mpango huo ya mwezi Agosti inaainisha kuhusu kuvunjiliwa mbali kwa kundi la waasi lililoasisiwa na viongozi wa zamani wa jamii ya Wahutu waliohusika na mauji ya halaiki ya Rwanda ya 1994 kama sharti muhimu la Rwanda kuwaondoa wanajeshi wake.