1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Congo yatangaza hatua mpya dhidi ya COVID 19

Admin.WagnerD17 Desemba 2020

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza hatua mpya za kupambana na wimbi la pili la maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19. Miongoni mwa hatua hizo ni kuwazuia watu kutoka nje kuanzia saa tatu usiku.

Kongo Kinshasa Félix Tshisekedi Präsident Kongo
Picha: Gislain Kusema/Press Office President DRC

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza hatua mpya za kupambana na wimbi la pili la maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19. Miongoni mwa hatua zitakazotekelezwa kuanzia kesho Ijumaa ni pamoja na kuwakataza wananchi kutembea kuanzia saa tatu usiku hadi saa kumi na moja asubuhi, na kupiga marufuku mikusanyiko ya watu zaidi ya kumi. 

Hatua hii ni uamuzi wa Rais wa Kongo, Felix Tshisekedi baada ya kukutana na wataalam wa masuala ya afya pamoja na wadau katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona, kwenye ikulu ya rais mjini Kinshasa.

Ongezeko la takwimu za hivi karibuni za maambukizi ndilo limempa hofu Rais Tshisekedi. Licha ya hatua za kupambana dhidi ya corona zilizopo tangu zamani, visa vipya vya ugonjwa huo zimezidi kuripotiwa nchini DRC hadi kufikia zaidi ya mia tatu kwa siku moja. Jolino Makelele ni msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kivu Kusini yashuhudia ongezeko la visa vya corona

This browser does not support the audio element.

Amesema ''Hatua zifuatazo zimechukuliwa: Kwanza; hakuna kutembea kuanzia saa tatu usiku hadi saa kumi na moja asubuhi. Pili; utekelezwaji madhubuti wa vitendo vya kuzuia maambukizi ya corona kama vile kuvaa barakoa, kutokaribiana sana na kadhalika. Tatu; maandamano, mikutano na shuguli za kitamaduni zimepigwa marufuku. Nne; pia mikutano ya zaidi ya watu kumi imepigwa marufuku. Tano; kuendelea kwa mashindano ya michezo huku milango ikiwa imefungwa. Sita; shughuli za mazishi zitafanyika papo hapo bila kuwepo  shughuli nyingine za ziadi.''

Shule kufungwa tena.

Tangazo hili pia limeiathiri sekta ya elimu. Kuanzia kesho Ijumaa, shule na vyuo zitafunga milango yake hadi tarehe isiyojulikana. Makanisa na vilabu vya pombe vitatumika kabla ya saa tatu usiku, kwa kuheshimu kanuni za kupambana na virusi vya corona.

Lakini hatua hii inatathminiwa tofauti na wakaazi, hasa wakati huu zinapokaribia sherehe za mkesha wa sikukuu ya Noeli na za mwisho wa mwaka.

Katika tangazo moja kwenye mtandao wa kijamii Facebook leo asubui, vuguvugu la vijana la LUCHA limekosoa pia hatua hii iliokusudiwa na Rais Tshisekedi na kutoa tahadhari kwamba janga la corona lisiwe kisingizio kwa kutekeleza ahadi ambazo rais huyo ametoa kwa raia wake muda mfupi uliopita. 

Soma Zaidi: Chanjo ya majaribio dhidi ya virusi vya Corona yazusha mjadala Congo

Mwandishi: Mitima Delachance