1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Congress Marekani yapitisha sheria kuibana Saudi Arabia

Admin.WagnerD29 Septemba 2016

Bunge la Marekani limepiga kura kupinga kura ya turufu ya Rais Barack Obama kuhusiana na sheria inayowapa nguvu wahanga wa mashambulizi ya Septemba 11 kuishitaki serikali ya Saudi Arabia.

USA Senat verhindert erstmals Veto von Obama
Picha: picture-alliance/AP Photo

Kwa mara ya kwanza, muswada huo wa sheria ulipigiwa kura katika baraza la Seneti ambapo wajumbe 97 walipiga kura kuipinga kura hiyo ya turufu, huku kura moja ikiunga mkono na baadaye kura kupigwa katika baraza la wawakilishi ambapo wajumbe 348 walipiga kura kuunga mkono kupitishwa sheria hiyo, huku wajumbe 77 wakiunga mkono kura hiyo ya turufu ya Rais Obama.

Kabla ya kura hiyo, Rais Obama alionya kuwa iwapo sheria hiyo itapitishwa na kuzipa nafasi familia za wahanga wa mashambulizi ya Septemba 11, basi itakuwa na athari kubwa kwa utendaji kazi wa wizara ya ulinzi ya Marekani, idara ya usalama wa taifa pamoja na masuala ya kidiplomasia yanayoihusu nchi hiyo.

Rais wa Marekani, Barack ObamaPicha: picture-alliance/dpa/M.B.Ceneta

Katika barua yake iliyowasilishwa kwa wajumbe wa chama cha Democrat pamoja na Republican katika baraza la Congress, Rais Obama alisema sheria hiyo haitasaidia kuwalinda Wamarekani dhidi ya mashambulizi ya kigaidi au kuimarisha mikakati ya kukabiliana na mashambulizi hayo. Aliongeza kuwa serikali ya Marekani inazo taratibu maalumu inazotumia katika kukabiliana na masuala ya aina hiyo.

Kwa upande wake, Chuck Schumer, mmoja wa maseneta walioupigania muswada huo, alisema kupitishwa kwa sheria hiyo kutasaidia kuzitendea haki familia za wahanga wa mashambulizi ya Septemba 11.

Ingawa watuhumiwa 15 miongoni mwa 19  waliohusika na mashambuklizi hayo nchini Marekani walikuwa ni raia wa Saudi Arabia, lakini bado hakuna ushahidi wowote unaotosheleza wa kuihusisha serikali ya Saudi Arabia na watuhumiwa hao.

Saudi Arabia, ambayo ni mshirika mkuu wa Marekani, imekuwa ikikanusha tuhuma hizo za kuhusika na mashambulizi hayo ya Septemba 11 ambayo yaliwaua kiasi ya watu 3,000 nchini Marekani.

Kwa upande mwingine, msemaji wa ikulu ya Marekani, Josh Earnest, alisema hatua ya kupitishwa kwa mswada huo limekuwa ni jambo la aibu kubwa kuwahi kufanywa na bunge la Congress katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita. Msemaji huyo ameongeza kuwa wajumbe wa Congress watawajibika kukabiliana  na yale yote yatakayojiri baadaye kutoka kwa wapiga kura wao kufuatia kupitishwa kwa sheria hiyo.

Hata hivyo, wanasheria wanaowawakilisha wahanga wa mashambulizi ya Septemba 11 wamepuuza hoja zinazoonesha kujenga hofu kuhusiana na kupitishwa kwa mswada huo, wakisem hazina msingi wowote.

Mwandishi: Isaac Gamba/DW English

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW