CONMEBOL yachukizwa na uamuzi wa FIFA
9 Mei 2020"Mabadiliko haya yametushangaza, hayakufanywa kwa mashauriano na shirikisho letu," Alejandro Dominguez (pichani) rais wa Shirikisho la soka la Amerika Kusini, CONMEBOL, aliandika katika mtandao wa kijamii wa twitter.
Mapema Ijumaa shirikisho la soka ulimwenguni FIFA liliziruhusu timu kuwa na wachezaji watano wa akiba kila mechi, badala ya watatu kama ilivyo kawaida, kama hatua ya muda kusaidia kukabiliana na msongamano wa ratiba za mechi huku mechi zikirejea baada ya kusitishwa kutokana na janga la virusi vya corona.
Mabadiliko hayo katika sheria yataruhusiwa katika mashindano yote yatakayokamilika mwishoni mwa mwaka 2020 na litakuwa jukumu la waandaaji wa mashindano hayo kuamua kuyatekeleza, ilisema FIFA.
Dominguez alisema shirikisho la CONMEBOL litaitisha kikao maalumu cha wataalamu kuuchambua uamuzi huo na kuamua kama unafaa kutumika katika mashindano ya Amerika Kusini kama vile Copa Libertadores.
(reuters)