1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Conservatives yapoteza ngome muhimu uchaguzi wa Uingereza

Sylvia Mwehozi
6 Mei 2022

Chama tawala cha kihafidhina nchini Uingereza, Conservatives, kimepoteza ngome zake muhimu mjini London katika uchaguzi wa serikali za mitaa na majimbo.

England | Premierminister Boris Johnson
Picha: Matt Dunham/AP Photo/picture alliance

Kulingana na matokeo ya awali ya uchaguzi ambayo yametangazwa siku ya Ijumaa. Matokeo hayo huenda yakaongeza shinikizo kwa Waziri Mkuu Boris Johnson katikati mwa kashfa za kimaadili na hali mbaya ya kiuchumi.

Uchaguzi huo uliofanyika siku ya Alhamisi kwa mabaraza zaidi ya 200 ulikuwa unachukuliwa kama kipimo cha maoni ya umma kuelekea uchaguzi mkuu ujao, ambao utafanyika mwaka 2024. Chama kikuu cha upinzani cha Labour ambacho kimekuwa nje ya madaraka ya kitaifa tangu mwaka 2010, kimeshinda udhibiti wa wilaya tatu za London za Wandsworth, Barnet na Westminster, ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikishikiliwa na chama cha Conservative.

Kiongozi wa chama cha Labour Keir StarmerPicha: Jonathan Brady/empics/picture alliance

Chama cha Johnson pia kimepoteza uungwaji mkono kwa chama cha Liberal Democrats kusini mwa Uingereza ambako chama cha Conservatives kilikuwa na ushawishi. Wapiga kura wengi wa tabaka la kati katika eneo hilo wanapinga Brexit na wamesikitishwa na kashfa ya kukiuka vizuizi vya Covid-19 na madai ya utovu wa nidhamu ya kingono yanayomzunguka Johnson na wanachama wengine waandamizi wa Conservatives.

Wakati matokeo ya karibu nusu ya England yakiwa yametangazwa kufikia Ijumaa, chama cha Labour hakikuwa kimepata ushindi mkubwa nje ya mji mkuu, hususan miongoni mwa tabaka la wafanyakazi kaskazini mwa England, maeneo ambayo Johnson alifanikiwa kushinda katika uchaguzi wa 2019 na kutoa ahadi ya kuboresha uchumi hasa baada ya Uingereza kujiondoa umoja wa Ulaya.

Mwenyekiti wa chama cha Conservatives Oliver Dowden amekiri kuwa matokeo jijini London yalikuwa "magumu" lakini akasema "picha zaidi tofauti" kwingineko zinaonyesha kwamba chama cha Labour hakijakuwa na nguvu ya kushinda uchaguzi mkuu.

Makamu rais wa chama cha Sinn Fein Michelle O'Neill Picha: Peter Morrison/AP/picture alliance

Mratibu wa kitaifa wa kampeni wa Labour Shabana Mahmood, amesema matokeo hayo yanadhihirisha kwamba chama chao kinajenga msingi thabiti wa kurejea madarakani baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu mara nne. "Labour inapiga hatua ... ikichukua nafasi muhimu ya mabaraza ya Conservatives na kushinda katika majimbo muhimu ya Bunge kote nchini''.

Kiongozi wa chama cha Labour Keir Starmer amesema "tumeleta mabadiliko ndani ya Labour na sasa tunashuhudia matokeo yake".

Matokeo zaidi yatazidi kutolewa siku ya Ijumaa kutoka kote England na Scotland pamoja na Wales. Huko Ireland ya Kaskazini, wapiga kura wanachagua bunge la viti 90, huku kura za maoni zikionyesha kwamba Chama cha kitaifa cha kizalendo cha Sinn Fein huenda kikapata wingi wa viti bungeni na kushika nafasi ya waziri mkuu, na hivyo kuandika historia.

Kampeni za uchaguzi zilitawaliwa na kuongezeka bei za vyakula na mafuta, ambazo zimepelekea gharama za kaya kupanda. Vyama vya upinzani vinaitaka serikali kuweka jizihada zaidi ili kupunguza hali mbaya ya gharama za  maisha inayochochewa na vita nchini Ukraine na janga la COVID-19 sambamba na athari za Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW