Conte aagizwa kuunda serikali mpya Italia
29 Agosti 2019Uamuzi huo umetolewa na Mattarella baada ya vyama viwili vya kisiasa nchini Italia, kile Nyota Tano na cha Democratic, kukubaliana kuunda serikali mpya ya mseto. Vyama hivyo vimeamua kuweka kando tofauti zao kuepusha uchaguzi ambao unaweza kumpa ushindi waziri wa mambo ya ndani wa siasa kali za mrengo wa kulia Matteo Salvini kama Waziri Mkuu.
Soma zaidi: Mchakato wa kuunda serikali ya muunano waendelea Italia
Muungano huo utaongozwa na waziri mkuu anayemaliza muda wake Giuseppe Conte, ambaye alijiuzulu wiki iliyopita kufuatia kuanguka kwa serikali yake mapema mwezi huu baada ya kukosa uungwaji mkono wa chama cha Salvini cha League.
Conte amelikubali agizo hilo na anatapewa siku chache za kufanya mashauri ya kisiasa kuhakikisha wingi kuhakikisha kwamba anapata wingi wa viti bungeni. Conte atahitaji kushinda kura ya imani kurudi tena madarakani kama Waziri Mkuu. Akipokea agizo hilo Conte lisema yafuatayo:
"Mimi ni profesa na wakili. Katika maisha yangu nimetetea watu wengi, sasa najitolea kutetea masilahi ya Waitaliano wote katika maeneo yote," amesema Conte.
Kiongozi wa Chama cha Nyota Tano Luigi Di Maio amesema mpango huo na chama cha Democratic utalazimika kupitishwa na wanachama wa chama chake kwa kura ya mtandaoni, ambayo inaweza kufanywa wikendi hii.
Salvini abeza
Wachambuzi wengi wanasema serikali inayoundwa na maadui wa kisiasa mara nyingi huwa haidumu muda mrefu.
Salvini ameubeza uwezekano huo wa kuunda serikali kati ya chama cha Nyota tano (M5S) na Democratic akisema kwamba hautadumu kwavile kitu pekee kinachowaunganisha ni chuki dhidi ya chama chake cha League.
Akirudia kile kinachosemwa na wachambuzi wengi, Salvini anatabiri kuwa muungano huo wa serikali utasambaratika muda mfupi baada ya kuundwa, na kutafanyika uchaguzi mkuu ndani ya miezi sita au mwaka mmoja ambao utampa yeye na chama chake ushindi.
Mapema jana, kiongozi wa chama cha Democratic, Nicola Zingaretti, alieleza kwamba kuridhia masharti ya chama cha Nyota 5 ya kumtaka Conte kurudi katika wadhifa wa waziri mkuu ni kwa maslahi ya wananchi wa Italia, kwani ndiyo itakuwa njia ya kukikinga chama cha League kuongoza serikali.
Zingaretti aliwaambia maripota kwamba ameshamueleza rais kwamba kwa vile Nyota Tano ni chama kikubwa zaidi bungeni, basi chama chake kitaunga mkono chaguo lao la waziri mkuu.
Bado haikuwekwa wazi vipi chama cha Democratic ambacho kinaunga mkono sera za Umoja wa Ulaya, kitaweza kuunda serikali ya mseto na chama cha Nyota Tano wanaochukia ushawishi wa Umoja wa Ulaya juu ya sera za kitaifa za Italia.
Chama hicho cha Democratic pia kilikuwa kikikosoa vikai msimamo wa kupinga wahamiaji nchini humo wa serikali ya Conte uliokuwa ukiongozwa na Salvini.
Chanzo: (afp,ap)