1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani ni nani katika serikali mpya ya Italia?

4 Septemba 2019

Italia imepata serikali mpya ya muungano ilioundwa na chama cha Nyota Tano (M5S) na chama cha mrengo wa wastani wa kushoto cha Demokratik (PD). Hawa ni baadhi ya wantedaji wakuu wa serikali mpya ya Italia.

Italien Rom Ministerpräsident Conte im Quirinalpalast
Picha: AFP/Quirinale Press Office

GIUSEPPE CONTE - WAZIRI MKUU

Ni profesa wa sheria mwenye umri wa miaka  55 ambaye amedhihirisha ujuzi mkubwa wa kunusurika kisiasa. Conte amebakia kwenye nafasi yake licha ya mabadiliko makubwa kwenye uwanja wa kisiasa nchini Italia.

Wakati Conte alipoteuliwa kuwa waziri mkuu kwa mara ya kwanza mwaka uliopita, aliongoza serikali ya siasa kali na yenye mashaka na Umoja wa Ulaya ambayo vuguvuvugu la Nyota Tano (M5S) liliiunda kwa kushirikiana na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha League.

Anarejea katika nafasi hiyo akiongoza serikali ya muungano kati ya M5S na chama cha Demokratik (PD), ambayo inatarajiwa kuwa na mikwaruzano kidogo na Umoja wa Ulaya na pia yenye msimamo laini kuhusu uhamiaji.

Rais Donald Trump alimuunga mkono Conte katika ujumbe wa twita wiki mbili zilizopita, akimuelezea kama mtu mwenye "heshima kubwa na mwenye ujuzi." Lakini alikosea jina la kwanza la Conte, na kumuita "Giuseppi."

Kiongozi wa chama cha M5S Luigi Di Maio ndiye amependekezwa kuwa waziri mpya wa mambo ya nje wa Italia.Picha: picture-alliance/ANSA/A. Di Meo

LUIGI DI MAIO - WAZIRI WA MAMBO YA NJE

Kiongozi huyo wa chama cha M5S mwenye umri wa miaka 33 ni mwenye nafasi ndogo ya kuwa waziri wa mambo ya nje kwa sababu hana ujuzi wowote wa lugha ya kigeni, ana hatari za kutoa matamshi ya fedheha, na anawakilisha chama chenye mitizamo kinzani kuhusu masuala ya kidunia.

Alishindwa kumaliza masomo ya chuo kikuu na anakejeliwa kwa kufanya makosa ya kisarufi katika lugha ya Kitaliana, huku chama chake cha M5S kikiwa na historia ya kubadilibadili misimamo kuhusu Umoja wa Ulaya, kanda ya Euro na jumuiya ya NATO kwa miaka kadhaa.

Mapema mwaka huu, Di Maio alisababisha mzozo wa kidiplomasia na Paris kwa kujaribu kuunda ushirikiano na vuguvugu la la maandamano la "Vizibao vya Njano."

Di Maio alikuwa naibu waziri mkuu na waziri wa viwanda na ajira katika serikali inayoondoka madarakani, na anasalia kuwa mtu muhimu katika serikali mpya kama kiongozi wa chama kikubwa zaidi katika muungano tawala.

ROBERTO GUALTIERI - WAZIRI WA UCHUMI

Mtu aliekabidhiwa mikoba ya idara inayoyumba ya fedha za umma ni profesa wa historia mwenye umri wa miaka 53 ambaye amejijengea utaalamu katika masuala ya kiuchumi na fedha wakati akihudumu kama mwanachama wa bunge la Ulaya kupitia chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha Democratic (PD).

Gualtieri amekuwa mwenyekiti wa kamati ya uchumi na fedha ya bunge la Ulaya tangu 2014, na ameshiriki katika majadiliano ya karibuni ya Burussels yanayohusisha masuala ya benki, kanda ya Euro pamoja na Brexit.

Roberto Gualtieri amekabidhiwa wadhifa wa waziri wa uchumi.Picha: picture alliance / AP Photo

LUCIANA LAMORGESE -WAZIRI WA MAMBO YA NDANI

Lamorgese ni mtaalamu ambaye atakuwa na wakati mgumu kubadili ukurusa juu ya sera kali na tata za uhamiaji zilizotekelezwa na mtangulizi wake, kiongozi wa chama cha mrengo mkali wa kulia cha League, Matteo Salvini.

Atatimiza miaka 66 ya kuzaliwa wiki ijayo. Ni afisa wa juu wa zamani katika wizara ya mambo ya ndani, nafasi inayohusisha kuongoza ofisi za serikali za mikoa nchini kote. Alishika wadhifa huo katika mikoa ya Milan na Venice.

Kama mrasimu wa wizara ya mambo ya ndani, Lamorgese ameshughulikia masuala ya utumishi na uhamiaji, na alikuwa katibu wa mawaziri kadhaa wa mambo ya ndani kuanzia 2013 hadi 2017. Lamorgese kwa sasa ni mjumbe wa mahakama ya juu ya utawala.

DARIO FRANCESCHINI - WAZIRI WA UTAMADUNI

Franceschini ni mwanasiasa wa muda mrefu na mwakilishi wa juu zaidi wa chama cha PD katika baraza la mawaziri la Conte. Uteuzi wake unaashiria kurejea kwake katika wizara ya utamaduni, baada ya kuwepo huko kwa miaka minne kuanzia 2014-2018.

Franceschini mwenye umri wa miaka 60 alianza kazi ya siasa mwishoni mwa miaka ya 1970 kama mdemokrat wa kikristu anaegemea mrengo wa kushoto. Alikuwa waziri mdogo katika serikali ya mrengo wa wastani wa kushoto kati ya 1999-2001 na kiongozi wa chama cha PD mwaka 2009.

Chanzo: dpae

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW