1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COP23: Nchi masikini zataka tajiri kujitwisha wajibu zaidi

Caro Robi
10 Novemba 2017

Nchi 134 zinazoendelea duniani zimeonya kuwa kukosa kwa nchi tajiri kutimiza wajibu wa kujitolea kufikiwa kwa malengo ya muda mfupi huenda kukahujumu juhudi za kuanza kutekelezwa kwa makubaliano ya kuyaokoa mazingira.

Deutschland Bonn COP23
Picha: DW/P. Große

Katika vikao vinavyoendelea katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira, hapa Bonn, nchi zinazoendelea zikiwemo China na India zimesema mivutano ya kidiplomasia inadhihirisha ugumu uliopo wa kufikia muafaka katika mazungumzo ya mazingira ya COP23 ambayo yanazileta pamoja nchi 196.

Mjumbe mkuu wa China katika mazungumzo hayo Chen Zhihua amesema iwapo maamuzi yaliyofikiwa kipindi cha nyuma hayaheshimiwi, basi inakuwa vigumu kujenga uaminifu miongoni mwa wadau.

Nchi tajiri zimetoa ahadi za kuimarisha ufadhili wa kifedha na kutathmini upya ahadi zao za kupunguza gesi chafu inayotoka viwandani kabla ya mwaka 2020, lakini masuala yote hayo mawili hayajapiga hatua.

Afrika yataka haki na usawa

Richard Muyungi, mkurugenzi wa mazingira katika Ofisi ya Makamo wa Rais Tanzania anasema suala la Afrika kusaidiwa kifedha linatizamwa kama haki ikizingatiwa mchango unaotoa katika kuyalinda mazingira.

Makubaliano yaliyofikiwa Paris, Ufaransa mwaka 2015, yanazitaka nchi kuchukua hatua za dharura na madhubuti kupunguza viwango vya joto hadi chini ya nyuzi mbili ikiwezekana hata iwe chini ya nyuzi 1.5.

Mjumbe wa China Wangn Shi katika mkutano wa COP23Picha: DW/M. Cui

Hivi sasa ulimwengu unashuhudia kuongezeka kwa viwango vya joto vilivyovunja rekodi ambavyo vimesababisha ukame hasa katika mataifa ya Afrika na kusababisha baa kubwa la njaa, watu kupoteza maisha yao, mifugo kufa, ardhi kutolimika na watu kulazimika kuyahama makazi yao na kwenda kwingine kutafuta chakula, maji, lishe kwa mifugo na vyanzo vingine vya kujitafutia riziki.

Pia mabadiliko hayo ya tabianchi yamesababisha joto kali katika nchi kama India, Pakistan na nchi za kiarabu huku nchi nyingine kama Marekani, Puerto Rico, za Pacifik na za visiwani zikikumbwa na vimbunga vikali na mafuriko makubwa yanayoharibu miundo mbinu na kusababisha maafa mengine makubwa.

Fiji ambayo ndiyo inashikilia urais wa kuandaa mkutano wa kimataifa wa mazingira imeonya kuwa inakabiliwa na gharama kubwa inayozidi kuongezeka ya kujilinda dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi na kuutaka ulimwengu kuchukua hatua zaidi kupunguza gesi ya Carbon ili kuweza kuzilinda nchi masikini na visiwani zinazokumbwa na kitisho cha mafuriko zaidi na vimbunga. Fiji inatumia asilimia kumi ya pato lake jumla la taifa kupamabana na majanga.    

Nchi zilizoendelea zapaswa kubeba mzigo mkubwa

Kuambatana na makubaliano yaliyofikiwa ya kuyalinda mazingira, mzigo mkubwa wa kufikia malengo yaliyowekwa ya muda mfupi ambao ni hadi mwaka 2020, unaziangukia nchi tajiri ambazo ndizo zinazochangia pakubwa katika uchafuzi wa mazingira kutokana na gesi chafu inayotoka katika viwanda vyao.

Kiwanda cha kuzalisha nishati ya makaa ya mawePicha: picture alliance/dpa

China ndiyo taifa linalochafua zaidi mazingira duniani kutokana na gesi ya Carbon, ikifuatiwa na Marekani, Nchi za Umoja wa Ulaya, India na Urusi. Nchi zinazoendelea kama za Afrika zinataka ajenda hiyo ya kufikiwa malengo ya 2020 kuongezwa rasmi katika mchakato wa mazungumzo ya COP23 lakini hatua hiyo iliwekwa kando mwanzoni mwa mazungumzo haya yatakayodumu kwa siku 12.

Juhudi za kusuluhisha tatizo hilo la kiasi gani cha fedha kitengwe kwa ajili ya kuzisaidia nchi masikini kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi nani atachangia nini na ni kwa kiasi kipi nchi zilizoendelea zitapunguza kiwango cha gesi chafu bado hazijafualu.

Kufikia sasa, kinachojiri katika vikao vya mkutano wa COP23 ni kunyoosheana vidole na mazungumzo hayo kuhusu mabadiliko ya tabia nchi kuanza kuchukua zaidi mkondo wa kisiasa. Wiki ijayo, takriban viongozi 20 wa nchi akiwemo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huu.

Mwandishi: Caro Robi/unfcc/afp/Reuters

Mhariri:Josephat Charo

https://cop23.unfccc.int/news/un-climate-change-announces-key-partners-supporting-cop23

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW