1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COP26: Viongozi wa dunia kujadiliana kudhibiti joto

31 Oktoba 2021

Wakuu wa mataifa wanakutana kwa ajili ya mkutano ya tabianchi, Glasgow. Mjadala mkubwa utaangazia mipango ya kupunguza matumizi ya mafuta ya petroli, kama namna pekee ya kuheshimu ahadi zao za kulinda sayari ya dunia.

Enlgland | COP26 | internationaler Klimagipfel in Glasgow
Picha: Scott Heppell/AP Photo/picture alliance

Wakuu wa mataifa na serikali wanakutana kwa ajili ya mkutano wa kilele wa mabadiliko ya tabianchi mjini Glasgow, Scotland. Mjadala mkubwa utaangazia mipango ya kupunguza matumizi ya mafuta ya petroli, kama namna pekee ya kuheshimu ahadi zao za kulinda sayari ya dunia.

Wakuu hao wa mataifa wanaokutana kwenye mkutano huo unaoanza leo hata hivyo bado wameshindwa kuweka sera zitakazozuia ongezeko la joto ulimwenguni kuwa chini ya kiwango cha joto cha nyuzi mbili, hali inayochukuliwa kama mwendelezo wa kushindwa kutekeleza makubaliano waliyoyafikia katika mkutano wa kilele wa Paris miaka sita iliyopita kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterress ameandika kupitia ukurasa wake wa twitter kabla ya mkutano huo kwamba iwapo serikali zote na hasa za kundi la mataifa yanayoinukia na yaliyoendelea kiuchumi, G20 hayataweza kusimama na kuongoza juhudi za kupambana na mzozo wa kimazingira, ni wazi pia kwamba ulimwengu unaelekea kwenye mzozo mwingine mbaya kabisa wa kibinaadamu.

Wanasayansi wanaonya kuhusiana na usambazaji wa gesi chafu kutokana na matumizi ya mafuta, ingawa maonyo yao yanapuuzwa.Picha: Nikolay Doychinov/AFP/Getty Images

Pamoja na maonyo yanayotolewa na wanasayansi kuhusiana na utoaji wa hewa chafu unaochangiwa na matumizi ya mafuta hayo katika miaka ya hivi karibuni, ambayo imeshuhudia matukio mabaya ya mabadiliko ya hali ya hewa na maandamano ya wanafunzi, lakini bado wanasiasa wanapuuzilia mbali maonyo hayo.

Soma Zaidi: Papa Francis: Mkutano wa COP26 lazima utoe matumaiani thabiti kwa vizazi vijavyo

Sasa, baada ya miongo miwili na nusu ya makubaliano, makumi kwa maelfu ya watu wanaelekeza macho yao huko Glasgow nchini Scotland katika mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi wa COP26. Mkutano huo unatajwa kuwa tumaini pekee la mwisho la kusimamisha ongezeko la joto duniani.

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema kabla ya mkutano huo kwamba "wakati mambo yakianza kuharibika, yanaharibika kwa kasi ya ajabu", na kufananisha mabadiliko ya tabianchi na anguko la uliokuwa utawala wa Roma.

'Ahadi hewa'

Mikutano ya kilele ya Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, ni majukwaa ya watawala wa dunia ya kukubaliana kuhusu mipango ya kupunguza matumizi ya mafuta. Zaidi ya makubaliano ya kiufundi, kama vile kanuni za mataifa kuripoti kuhusu namna yatakavyopunguza uchafuzi wa hewa ama watakavyofanikisha makubaliano yaliyopita, washiriki watajadiliana kuhusu masuala mawili muhimu: usambazaji wa gesi chafu na fedha.

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameonya kuhusu umuhimu wa kuchukua hatua za haraa kupambana na mabadiliko ya tabianchi.Picha: Jon Super/AP Photo/picture alliance

Uingereza ambayo ni mwenyeji wa mkutano huo inashinikiza viongozi kuahidi kupunguza usambazaji wa hewa ukaa kwa haraka zaidi. Imeyaweka masuala ya makaa ya mawe, magari, fedha taslimu na miti kama ajenda muhimu kwenye mkutano huo. Mataifa tajiri yameshindwa kutimiza ahadi walizotoa kwenye mkutano kama huo uliopita wa kuyalipa mataifa masikini zaidi dola bilioni 100 kila mwaka, katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabiancho ifikapo mwaka 2020.

Baadhi ya wajumbe wa mataifa hayo masikini na yaliyo hatarini zaidi, ambao miongoni mwao wameshindwa kuhudhuria mkutano huo kutokana na vizuizi vya corona ama hali mbaya ya kifedha wametoa wito kwa mataifa tajiri kulipia athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi kwasababu ya kuchangia katika tatizo hilo kwa kiasi kikubwa.

Soma Zaidi: Viongozi wa G7 kuongeza fedha za kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi

Wanasayansi, wanaharakati na wajumbe wanaoongoza mapambano haya wanatilia shaka uwezo wa mikutano kama hii wa kusuluhisha matatizo, na wamekuwa wakiyakosoa mataifa tajiri kwa kushindwa kuheshimu ahadi zao.

Pamoja na yote, bila ya kuwepo kwa mabadiliko ya kisera katika nyakati hizi, wanasayansi wanasema sayari ya dunia huenda ikakabiliwa na viwango vibaya kabisa vya joto. Kabla ya makubaliano ya Paris, dunia ilikuwa ikielekea kuwa na ongezeko la joto la karibu 4 C. Lakini iwapo ahadi zitatekelezwa, viwango hivyo vitaishia 2 C hadi 2.5 C ifikapo mwishoni mwa muongo huu.

Mashirika: DW

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW