1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COP27: Kiwango cha uzalishaji gesi chafu kiko juu kabisa

11 Novemba 2022

Wanasayansi wanasema kiwango cha utoaji wa gesi chafu zinazoharibu tabaka hewa kinaelekea kupanda kwa asilimia moja mwaka huu, hali ambayo itafanya iwe vigumu kwa dunia kukwepa majanga ya kimaumbile katika siku zijazo

COP27 Leah Namugerwa Rede
Picha: Sean Gallup/Getty Images

Ripoti iliyowasilishwa siku ya Ijumaa (Novemba 11) kwenye mkutano wa COP27 kwa jina Bajeti ya Hewa ya Ukaa Ulimwenguni iliweka bayana pengo kubwa lililopo baina ya ahadi zinazotolewa na serikali, kampuni na wawekezaji kupunguza kiwango cha uzalishaji wa hewa chafu siku zijazo na vitendo vyao halisi vya sasa, ambavyo vinasababisha uchafu huo kuongezeka.

Ripoti hiyo ilisema kuwa nchi zinatazamiwa kuondosha tani bilioni 41 vya hewa ya ukaa mwaka wa 2022, kati yake zikiwa tani bilioni 37 kutokana na nishati za visukukuna bilioni nne kutokana na matumizi ya ardhi kama vile ukataji wa misitu.

Lakini wanasayansi waliowasilisha ripoti hiyo mbele ya mkutano wa COP27 mjini Sharm Al Sheikh walisema, badala yake, kumekuwa na ongezeko la hewa chafu lililochangiwa na matumizi makubwa ya mafuta - hasa kwenye sekta ya usafirishaji wa anga - wakati chumi zilipoanza kurejea hali ya kawaida baada ya janga la UVIKO-19.

Uchafu unaotakana na makaa ya mawe pia umeongezeka, wakati mataifa kadhaa yakirejea kwenye nishati hiyo hatari kabisa kwa usalama wa mazingira kufuatia vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine, ambavyo vimepandisha bei ya gesi ulimwenguni.

China yapunguza kuchafuwa mazingira

Picha: Mohammed Abed/AFP

Hata hivyo, wanasayansi hao walisema China, taifa linaloongoza kwa kuchafua mazingira duniani, mwaka huu limeshusha kiwango chake cha utoaji wa gesi chafu hadi chini ya asilimia moja wakati ikiendelea na operesheni yake ya kusambaa kwa maambukizo ya virusi vya korona. 

Hali ni sawa na Ulaya ambayo nayo imepunguza kasi yake ya uchafuzi wa mazingira kupitia uzalishaji wa gesi chafu.

Lakini Marekani - ambayo ni ya pili kwa uchafuzi wa tabakahewa - imeongeza kiwango cha utoaji wa gesi hiyo hadi asilimia 1.5, huku India - inayoshikilia nafasi ya nne ya uchafuzi - ikichupa hadi asilimia 6. 

Lazima gesi chafu ipunguwe

Baadhi ya washiriki wa mkutano wa mabadiliko ya tabianchi, COP27, nchini Misri.Picha: MOHAMMED SALEM/REUTERS

Jopo la sayansi ya mabadiliko ya tabianchi la Umoja wa Mataifa lilisema kiwango cha gesi chafu kwenyetabakahewa lazima kishuke kwa asilimia 43 ifikapo mwaka 2030 ili kulifanya joto ulimwenguni lisipindukie nyuzi 1.5 na kuepuka majanga mabaya ya kimaumbile. 

Wakati janga la UVIKO-19 lilisababisha kushuka kwa kasi kubwa uzalishaji wa gesi chafu duniani mwaka 2020, uzalishaji huo sasa umeanza kuja juu tena kupindukia hali ilivyokuwa kabla ya janga la virusi vya korona kuanza. 

Glen Peters, mkurugenzi wa utafiti katika taasisi ya utafiti wa mabadiliko ya tabianchi ya Norway, CICERO, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba "uchafu kutokana na mafuta unachangiwa pakubwa na kurejea kwa shughuli za kawaida baada ya janga la UVIKO-19, huku ule wa gesi na makaa ya mawe ukichangiwa na vita nchini Ukraine."

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW