COP27: Mkutano wa kilele kuhusu hali ya hewa wamalizika
19 Novemba 2022Mkutano wa kilele wa COP27 sasa unasubiriwa kuridhia kuzinduliwa hazina hiyo mpya ya kuzisaidia nchi kukabiliana na gharama ya uharibifu unaoletwa na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Wajumbe kutoka karibu nchi 200 katika mkutano wa kilele wa COP27 unaofanyika nchini Misri sasa watazingatia na kuangalia uwezekano wa kufanya mabadiliko kabla ya kuamua kuiidhinisha rasimu hiyo inayodhamiria kuanzishwa kwa fuko la fedha kwa ajili ya kukabiliana na hasara na uharibifu kutokana na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Soma zaidi:COP27: Kiwango cha uzalishaji gesi chafu kiko juu kabisa
Wito wa nchi zinazoendelea wa kuanzishwa kwa hazina kama hii ulitawala mazungumzo ya Umoja wa Mataifa katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, na kusababisha kuongezwa muda wa mkutano huo wa kilele uliiopangiwa kufikia mwisho wake siku ya Ijumaa huku nchi zikihangaika kufikia makubaliano.
Nchi za Umoja wa Ulaya zaashiria utayari wa kufikia maelewano kuhusu ufadhili kwa nchi zilizo hatarini.
Rasimu iliyopendekezwa inalenga kuondoa utata juu ya maamuzi ya mfuko katika mwaka ujao, wakati ambapo kamati ya mpito itatoa mapendekezo kwa nchi za ulimwengu ambayo yatatarajiwa kuzingatiwa na kupitishwa katika mkutano wa kilele wa hali ya hewa wa COP28 utakaofanyika mwezi Novemba mwaka ujao wa 2023.
Wajumbe kwenye kutano wa COP27 wamesema ni vizuri kufikia makubaliano ya kuanzishwa hazina ya kuyalipa fidia mataifa maskini ambayo yanaathiriwa na hali mbaya ya hewa kutokana na uharibifu wa hali ya hewa ambapo mataifa tajiri ndio wachafuzi wakubwa wa mazingira.
Soma zaidi:COP27: Guterres atoa wito wa kufikia makubaliano katika Mkutano wa Mazingira
Alex Scott, mtaalam wa diplomasia ya hali ya hewa katika jopo la watalaamu la E3G, amesema rasimu hiyo ikiidhinishwa, itakuwa ni ushindi mkubwa kwa mataifa maskini ambayo yamekuwa yakitoa miito ya kupewa fidia kwa miongo kadhaa kwa sababu mataifa hayo ndio waathirika wa majanga ya hali ya hewa licha ya kuchangia kwa kiwango kidogo katika uchafuzi wa mazingira unaosababisha ongezeko la joto duniani.
Yeb Sano, Mkuu wa ujumbe wa walinzi wa mazingira, Greenpeace katika mkutano wa COP27 kwa mara nyingine tena ametoa wito kwa Misri ambayo inashikilia urais wa mkutano huo, kukataa ushawishi wa mataifa yanayozalisha mafuta na wapiga debe wa nishati nza mafuta, makaa ya mawe na gesi ili malengo ya COP27 yafanikiwe.
Vyanzo:RTRE/AP