1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COP27: Ukataji miti waongezeka Bonde la Kongo

10 Novemba 2022

Wataalamu wa mazingira wamesema ukataji wa miti katika msitu mkubwa wa Bonde la Kongo umeongezeka kwa asilimia tano kwa mwaka 2021.

Demokratische Republik Kongo | Gerodeter Wald nahe Kisangani
Picha: SAMIR TOUNSI/AFP/Getty Images

Ripoti ya Tathmini ya Azimio la Misitu iliyotolewa Alhamisi imeeleza kuwa ni nchi mbili tu kati ya sita za Bonde la Kongo ambazo zimesaini makubaliano ya kusitisha na kupunguza ukataji wa miti ifikapo mwaka 2030. Congo na Gabon ndizo zinazolengwa zaidi. Ripoti hiyo imetolewa wakati maafisa na wapatanishi wakiendelea na mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira COP27 kwenye mji wa mapumziko wa Sharm el-Sheikh nchini Misri.

Marion Ferrat, mwandishi mkuu wa ripoti hiyo, amesema msitu wa Bonde la Kongo uko katika njia panda na kwamba hali hiyo ikiendelea, kuna hatari ya kupoteza msitu mkubwa zaidi uliosalia pamoja na thamani yake kubwa na isiyoweza kubadilishwa kwa viumbe hai, hali ya hewa na watu.

Dola bilioni 100 zahitajika kuilinda Amazon

Lawrence Nsoyuni wa kampuni ya teknolojia ya Geospatial anasema inakadiriwa kuwa dola bilioni 100 zinahitajika ili kulihifadhi Bonde la Amazon kila mwaka.

Huku hayo yakijiri wanaharakati wa mazingira wamekusanyika katika eneo unakofanyika mkutano wa COP27 kupinga uchafuzi wa hali ya hewa.

Wakizungumza katika maandamano hayo, wanaharakati wamewalaumu wachafuzi wakubwa wa hali ya hewa ambao matokeo yake ni kutokea kwa mafuriko, ukame na kuongeza kwa viwango vya bahari. Wamesema wanasimama na watu wao kufikiria kuhusu sayari yao na hivyo wanatetea haki yao irudishwe.

Wanaharakati wa mazingira wakiandamana huko Sharm el-Sheikh, MisriPicha: Sean Gallup/Getty Images

Wakati huo huo, mazungumzo ya ngazi ya juu kuhusu kuongezwa kwa ufadhili katika nchi maskini kwa lengo la kukuza uchumi wao wa kijani na kujiandaa kwa athari za ongezeko la joto duniani yalianza Jumatano, huku wajumbe wa majadiliano hayo wakitofautiana kuhusu ukubwa wa ufadhili na watoaji.

Nchi zilizoendelea ambazo zinahudhuria mkutano wa COP27 zimesema lengo la dola bilioni 100 litafikiwa hadi mwishoni mwa mwaka 2023. Mazungumzo yanaendelea pia kuhusu kiasi gani cha kutoa baada ya awamu ya sasa ya ahadi kumalizika ifikapo mwaka 2025, na iwapo waongeze idadi ya wafadhili ili kuzijumlisha nchi nyingine, hasa China.

Nchi zinazoendelea zakosoa kukosekana usawa

Viongozi kutoka katika nchi zinazoendelea zimekosoa ukosefu endelevu wa usawa katika ufadhili wa hali ya hewa ambao ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, unapaswa kugawanywa kwa usawa kati ya kupunguza uchafuzi, na kuimarisha uthabiti kwa ajili ya madhara ya baadae.

Ama kwa upande mwingine, Rais wa Uganda Yoweri Museveni amezishutumu nchi za Ulaya kwa kuwa na ''hali ya undumilakuwili'' kuelekea Afrika katika sera zake za hali ya hewa na nishati. Katika makala yake kwenye blogu moja iliyochapishwa jana Jumatano, Museveni amesema hawatokubali sheria moja kwa Ulaya na nyingine kwa Afrika.

Aidha, nchi sita za bara la Asia zimeokoa takribani dola bilioni 34 kwa mwaka huu kwa kutumia nishati ya jua badala ya vyanzo vichafu vya nishati kama vile mafuta na makaa ya mawe. Hayo yamebainishwa Alhamisi katika ripoti ya mashirika matatu ya wataalamu wa masuala ya hali ya hewa yenye makao yake Asia.

(AP, AFP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW