COP30: Mafanikio ya miaka 10 ya mkataba wa Paris
13 Novemba 2025
Hata hivyo, ukuaji wa nishati ya jua, upepo na magari ya umeme unaonyesha kuwa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinaweza kufanikiwa. Je, nini kimefanikiwa na kipi kinasalia kufanywa kwa dharura ili kupata mafanikio zaidi?
Baada ya kufikiwa makubaliano hayo ya Paris mwaka 2015, viongozi wa dunia walishikana mikono na washiriki wa mkutano wa mazingira wa Umoja wa Mataifa wa COP21 na walionekana wenye furaha na kupongezana kwa kufikia hatua hiyo.
Makubaliano hayo yaliashiria kufikiwa hatua muhimu katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mara ya kwanza, takriban mataifa 200 yalipitisha mkataba wa kupunguza ongezeko la joto duniani hadi kufikia nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Celcius ukilinganisha na viwango vya kabla ya mapinduzi ya kiviwanda.
Wanasayansi wanasema kufikiwa kiwango hicho ni muhimu ili dunia ijikinge na madhara makubwa yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi, lakini Umoja wa Mataifa sasa umesema kuwa kuvuka kiwango hiki, angalau kwa muda, ni jambo lisiloepukika na litakuwa na "athari mbaya” kwa ulimwengu.
Licha ya hatua kubwa zilizopigwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, wataalamu bado wanatahadharisha kuwa dunia ipo katika kipindi kigumu na muhimu.
Huku baadhi ya mataifa yakiendelea na matumizi ya nishati ya visukuku kama mafuta, gesi na makaa ya mawe, joto linaongezeka, na kusababisha dhoruba, mafuriko na joto kali. Muongo uliopita ulikumbwa na aina mbalimbali za majanga ya asili.
Viwango vya joto vimepanda tangu Makubaliano ya Paris
Wakati viongozi wa dunia wakikusanyika katika mji wa Belem, huko Brazil kwa mkutano wa kimataifa wa mazingira wa COP30,
uzalishaji wa gesi chafu unaongezeka na ulifikia viwango vya juu kuliko vile vya mwaka 1990.
Ili kufikia malengo ya makubaliano hayo ya Paris, uzalishaji wa gesi chafu unapaswa kupunguzwa maradufu licha ya kutokuwa na dalili zozote za kulifikia lengo hilo.
Bila ya kufikiwa makubaliano hayo, joto la dunia lilitarajiwa kufikia nyuzi joto 4 celcius mwishoni mwa karne hii.
Makubaliano hayo yanazitaka nchi kuwasilisha mipango yao ya kitaifa kuhusu hatua zinazochukuliwa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Ikiwa mipango hiyo itatekelezwa kikamilifu, dunia itafanikiwa kudhibiti ongezeko la joto na kufikia nyuzi joto 2.3 hadi 2.5. celcius.
Kabla ya mkutano huu wa COP30, mataifa mbalimbali yalikuwa bado yanahangaika kuwasilisha ahadi zao mpya za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Utafiti mpya wa Umoja wa Mataifa kuhusu ahadi za kitaifa, unakadiria kuwa uzalishaji wa gesi chafu duniani utapungua kwa takriban asilimia 12 kufikia mwaka 2035 ikilinganishwa na viwango vya mwaka 2019.
Dunia inahitaji kuona kasi kubwa mno ya kuzidisha malengo ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafu katika sekta zote.