Copa America laendelea-Kombe la Asia laanza:
6 Julai 2007
Timu kali za bara la Asia:mabingwa Japan,Korea ya Kusini,Iran na hata Saudi Arabia ambazo zote zilishindwa kutamba katika kombe lililopita la dunia nchini Ujerumani mwaka uliopita,zinataka kuoneshana mnamo wiki hizi 3, nani hasa ni bingwa.
Kombe la bara la Asia, limeandaliwa kwa ubia na nchi 4 mbali mbali:Hii imeliumiza kichwa shirikisho la dimba la Asia, huku pakiwapo pia vituo 4 vya waandishi habari.
Australia,mabingwa watetezi, Japan,Korea ya Kusini na Saudi Arabia mojawapo kati ya hizo yapigiwa upatu kutwaa ubingwa.
Mwanachama mpya Australia,itataka kutamba mara ya kwanza ikishiriki katika kombe hilo baada ya kuhama kutoka shirikisho la CONCACAF.
Kwahivyo, ikiwa kombe lililopita la bara la asia 2004 ni kiyoo cha kumurika changamoto za mwaka huu zitakuaje huko Thailand,basi kuna mengi ya kutazamia.
Pale kombe hili lilipochezwa nchini China miaka 3 iliopita,makocha walitimuliwa ,mashabiki walizusha fujo,wachezaji walipigana ngumi na kadi 17 nyekundu zilitolewa n a hata siasa iliingizwa katika dimba.
Thailand imefungua dimba leo na Iraq katika uwanja wa Taifa wa Rajamangala, mjini Bang Kok.Usalama umeimarishwa huku polisi ikionya na mapema kuwa usalama wa wachezaji na mashabiki mnamo wiki 3 zijazo ni jambo la kwanza kabisaa.
Mabingwa Japan watazamiwa kutamba katika kundi B linalojumuisha Umoja wa falme za Kiarabu (Emirates),Qatar na mwenyeji-mwengine wa kombe hili- Vietnam.
China imejiandaa barabara kwa kombe hili katika kundi C ; na ndio iliocheza finali mara iliopita.Mahasimu wao ni wenyeji wengine-Malaysia kabla hawakukumbana na Iran na halafu Uzbekistan .Katika kundi D, kuna Korea ya kusini,waliocheza nusu-finali ya kombe la dunia nyumbani 2002.Wanakutana na Saudi Arabia,Bahrein na Indonesia.
Timu 16 zinashiriki katika Kombe la Asia sawa na ilivyo katika Kombe la Afrika la mataifa litakaloaniwa Januari mwakani nchini Ghana.Mechi 32 zitachezwa kabla hawakuibuka mabingwa.
Kombe la bara la Asia-Asian Cup lilianzishwa 1956 na mabingwa wakawa Korea ya Kusini waliorudi tena miaka 4 baadae kutetea taji lao.
1964 ikawa zamu ya Israel kutwaa kombe,enzi yao lakini ikakomeshwa na Iran iliolinyakua kombe hilo mara 3 mfululizi-1968,1972 na 1976.
1980 ikawa zamu ya kuweit kabla majirani zao Saudi Arabia kuingiwa nao na uchu wa kombe hilo na kulitwa hadi Riyadh, 1984.Utamu ulipowakolea wasaudi hawsakulitoa walibakia nalo 1988.Japan ilikomesha enzi yao 1992 lakini wasaudi wakalinyakua tena 1996.
Miaka 8 iliofuatia ikawa zam,u ya japan-mwaka 2000 na 2004.Japan wamevinjari kuridi na kombe hilo Tokyo.Lakini kuna Waustralia wanaolitaka kwa hamu kulichukua nyumbani mara ya kwanza wakishiriki.
Sambamba na Kombe la Asia, kinyan’ganyiro cha Copa America –kombe la Amerika kusini kinaendelea nchini Venezuela na timu zote za robo-finali sasa zinajulikana :
Iliokata kwanza tiketi yake ilikua Mexico iliofungua dimba kwa kuwaibisha mabingwa Brazil kwa mabao 2:0.
Robo-finali ya Copa America, inawakutanisha leo wenyeji Venezuela na Uruguay-mabingwa wa kwanza kabisa wa kombe la dunia,1930.Changamoto hii, inachezwa San Crristobal. Mabingwa -Brazil wana miadi na Chile huko Puerto La Cruz.
Kesho jumapili, itakua zamu ya Mexico kuumana na Paraguay huko Maturin.
Macho ya mashabiki lakini yataukodolea macho mpambano kati ya Argentina na Peru uwanjani Barquisimeto.
Kabla kuanza kombe hili la Amerika, upatu ukipigiwa na kuhanikiza kwamba, Argentina ingeivua taji Brazil na kutawazwa wao mabingwa wapya wa Amerika.Na Argentina haikuvunja moyo ,kwani ndio timu pekee hadi sasa isiopoteza hata pointi moja na imeshinda mapambano yake yote 3 ya kwanza.
Kesho basi Peru, itakiona kilichomtoa kanga manyoya.Brazil imepepesuka na kuingia nayo robo-finali ya kombe hili kutokana na mabao 4 ya Robinho.
Nyumbani kocha Dunga amekosolewa sana baada ya Brazil kumudu ushindi wa bao 1:0 dhidi ya Ecuador-bao la penalty.Dunga amekosolewa pia kwa kuteremsha wachezaji 3 wa kiungo wakujilinda.Gazeti la michezo la Brazil-Kance-limechapiasha picha ya chipukizi Robinho na kichwa cha maneno:ANGALIA NANI AIOKOKA BRAZIL ?”Robinho.
Wachezaji wa Brazil lakini wanadai hawana wasi wasi na kile ambacho vyombo vya habari nyumbani vimeita “mchezo wao usiopendeza”.Brazil imeingia robo finali kupitia mlango wa nyuma-nafasi ya pili katika kundi lililooongozwa na Mexico.
Brazil yadai-“kutangulia si kufika”.
Kombe la vijana la dunia chini ya umri wa miaka 20 likiendelea nalo nchini kanada, Kongo imezabwa mabao 3:0 na Chile wakati Austria imeizima kanada wenyeji kwa bao 1:0.Gambia imemudu ushindi mbele ya New Zealand wa bao 1:0 lakini, Ureno ilizama kwa mabao 2:1 mbele ya Mexico kabla timu kurudi uwanjani mwishoni mwa wiki hii:
Mzee Nelson Mandela, ataadhimisha siku ya kuzaliwa akitimu umri wa miaka 89 hapo julai 18.
Shirikisho la dimba la dunia-FIFA lapanga kutoa tunzo maalumu kwa wafungwa wa gereza la kisiwa cha Robben, Island nchini Afrika kusini.rais wa FIFA Sepp Blatter atatoa siku hiyo uanachama wa heshima kwa chama cha mpira cha Makana Football Association –chama kilichoundwa na wafungwa enzi za utawala wa ubaguzi na mtengano –aparthied.
Mzee Mandela alipitisha miaka 18 kati ya kifungo chake cha miaka 27 kisiwani humo.JUlai 18 timu 2 zitateremka uwanjani timu ya bara la afrika ya mchanganyiko nay a dunia huko Cape Town.
Nje ya medani ya dimba, baada ya mji wa Urusi wa sochi kuchaguliwa kati ya wiki hii kituo cha michezo ya Olimpik ya majira ya baridi 2014, mji wa munich-kituo cha michezo ya Olimpik ya majira ya kiangazi 1972, umetangaza kugombea kuandaa michezo ya majira ya baridi 2018-miaka 4 baada ya Sochi.
Kwa vijana chipukizi,Halmashauri kuu ya olimpik Ulimwenguni-IOC iliidhimnisha pia mpango wa kuandaa michezo ya kwanza ya olimpik kwa chipukizi ili kuzuwia kupunguka kwa hamu kwa vijana na michezo ya olimpik.
Wanariadha kati ya umri wa miaka 14-18 watashiriki katika michezo ya kwanza ya majira ya kiangazi hapo 2010 na ile ya majira ya baridi itakua miaka 2 baadae.
Michezo ya olimpik imefanyika katika mabara yote isipokua afrika.Ni matarajio ya Waafrika alao michezo hii ianze barani humo.Kombe la kwanza la dunia la FIFA nchini Afrika kusini 2010 litatoa mwangaza iwapo ndoto hiyo pia ya olimpik itatimilia siku moja barani Afrika.