1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona: Idadi ya vifo ulimwenguni yafikia watu 60,000

Zainab Aziz Mhariri: Sylvia Mwehozi
4 Aprili 2020

Watu waliokufa baada ya kupata ugonjwa wa COVID -19 ulimwenguni kote imefikia watu elfu 60. Zaidi ya watu milioni moja na laki moja wamethibitishwa kuwa wameambukizwa na virusi hivyo katika nchi 190 duniani kote.

Spanien Leganes | Coronavirus | Patient Notaufnahme
Picha: Reuters/S. Vera

Italia na Uhispania ndio zimekumbwa zaidi na janga la virusi vya corona wakati ambapo nchi za Ulaya zinapambana na janga hili la maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19. Italia iliripoti mtu wake wa kwanza kufa kutokana na ugonjwa wa COVID -19 mnamo mwishoni mwa mwezi Februari, hadi sasa nchi hiyo imeorodhesha vifo 14,681 huku watu wapatao 119,827 wakiwa wamembukizwa virusi hivyo. Watu 19,758 walitibiwa na kupona.

Ujerumani imethibitisha kwamba maambukizi yameongezeka katika muda wa saa 24 zilizopita na kufikia watu 6,082 kwa mujibu wa taasisi ya Robert Koch (RKI). Mkuu wa taasisi ya Robert Koch Lothar Wieler amesema jimbo la Bavaria sasa lina afadhali kwa kuwa maambukizi yamepungua kidogo. Kulingana na takwimu za taasisi ya Robert Koch idadi ya watu waliokufa hata hivyo imeongezeka na kufikia watu 1,158.

Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema zuio la kitaifa linalowataka watu wabakie nyumbani huenda likaendelea hadi baada ya kipindi cha Pasaka. Hata hivyo Ujerumani imeeleza wasiwasi juu ya kuongezeka matukio ya vurugu majumbani kutokana na hatua za kubakia nyumbani zilizowekwa.

Wakati huo huo daktari wa kitengo cha wagonjwa mahututi mjini Paris nchini Ufaransa Jean-Paul Mira ameomba msamaha baada ya siku ya Ijumaa kupendekeza chanjo ya kifua kikuu ifanyiwe majaribio barani Afrika kubaini kama inaweza kutumiwa kupambana na ugonjwa wa  COVID-19. Daktari huyo aliyasema hayo kwenye kipindi cha majadiliano na mtaalam mwenzake kwenye runinga.

Kauli hiyo ilizua hisia za ghadhabu na kujibiwa na watu mbalimali akiwemo nyota mstaafu wa mpira wa miguu wa Ivory Coast, Didier Drogba kwamba Afrika sio maabara ya kufanyia uchunguzi, na mwakilishi wa mawakili wa Moroko amesema chama cha mawakili kitamshtaki daktari Mira kwa kuwadunisha watu katika misingi ya ubaguzi wa rangi.

Kundi la Ufaransa la kupambana na ubaguzi wa rangi -SOS Racisme limesema Waafrika sio wanyama wa majaribio na taasisi ya maadili ya utangazaji nchini Ufaransa CSA imesema imepokea malalamiko.

Mtandao wa hospitali ya Cochin ambapo Mira ndiye mkuu wa kitengo hicho cha kuwahudumia wagonjwa mahututi mjini Paris, siku ya Ijumaa ulimnukuu daktari Mira akisema: "Nataka kuwasilisha ombi langu la kutaka kusamehewa kwa wote ambao wameumizwa, wamekwazika na wamehisi kutukanwa na maneno niliyoyasema ."

Vyanzo:/AFP/RTRE/DW

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW