1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Italia yaipita China kama nchi yenye idadi kubwa ya vifo

20 Machi 2020

Uingereza imewaomba madaktari wastaafu kurudi kazini ili kusaidia kukabiliana na janga la Corona huku waziri mkuu wa Italia akitoa wito kwa Umoja wa Ulaya kutumia uwezo wake imara wa kifedha kupambana na janga la Corona.

Italien Rom | Coronavirus | Giuseppe Conte, Ministerpräsident
Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe ContePicha: Reuters/R. Casilli

Baraza la wauguzi na wakunga nchini Uingereza limewaandikia barua zaidi ya wauguzi 50,000 pamoja na madaktari 15,000 waliostaafu ili kuwarai kurudi kazini kwa ajili ya kusaidia kupambana na janga la virusi vya Corona.

Kadhalika wanafunzi wanaosomea taaluma ya matibabu ambao wako mwaka wao wa mwisho pia wamepewa nafasi muhimu kutumia ujuzi wao kukabiliana na virusi hivyo.

Kwa sasa idara ya afya nchini Uingereza inaweka wazi vitanda 30,000 kwa kuahirisha oparesheni zisizohitaji udharura na pia kutoa huduma za kijamii kwa wagonjwa ambao wanakaribia kupata nafuu. Vilevile, idara hiyo ya afya imesema inatafuta hospitali za kibinafsi na za kijamii 10,000 ili kukidhi mahitaji ya dharura. Hatua zote hizo zimechukuliwa kwa ajili ya kushughulikia janga la hivi sasa la Corona.

Afisa mkuu wa wauguzi nchini humo Ruth May amesema: "Hatuwezi kufanikiwa katika hili pekee yetu, ninatoa wito kwa wauguzi wastaafu kutusaidia wakati huu wa mlipuko wa virusi vya Corona kwa sababu nina amini kuwa munaweza kutusaidia kuokoa maisha"

Wauguzi nchini UingerezaPicha: picture-alliance/dpa/empics/PA Wire/O. Humphreys

Na nchini Italia, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Giuseppe Conte ameutolea wito Umoja wa Ulaya kutumia uwezo wao imara wa fedha kupambana na mlipuko wa Corona.

Katika mahojiano na gazeti la Financial Times, Conte ametaka Umoja wa Ulaya ubadilishe utaratibu wake wa kutoa mikopo hasa kwa nchi zenye kutumia sarafu za Euro na ambazo zinakabiliwa na madeni ili kuzisaidia kupambana na janga hilo.

Ursula von der Leyen ni Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya: "Nina habari nzuri kwa Italia. China iko tayari kutuma barakoa milioni 2. Kati ya hizo, laki mbili ni barakoa maalum. Pia viko vifaa vya upimaji elfu 50. Tunatuma zote hizo kama Umoja wa Ulaya kwa sehemu inayohitaji zaidi msaada nayo ni Italia. Vifaa hivyo vikitufikia, tutavituma vyote wiki ijayo nchini Italia.

Nchi hiyo imefunga na kusimamisha shughuli katika bandari zake katika hali ya kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona. Wizara ya uchukuzi imeziagiza meli ambazo tayari ziko baharini kurudi bandarini na watu wote kufanyiwa vipimo.

Idadi jumla ya vifo vilivyotokana na Corona nchini humo vilipindukia ile ya China kufikia jana Alhamisi. Kwa sasa, vifo vilivyotokana na virusi vya Corona vimefikia 3,405 nchini humo.

Na nchini Ufaransa, serikali imewaondolea hofu wafanyakazi kwa kusisitiza kuwa ina fedha za kutosha kuiwezesha kulipa mishahara ya wafanyakazi wake wakati huu wa janga la Corona. Waziri wa fedha Bruno Le Maire amesema hayo kupitia runinga ya LCI.

 

 

Vyanzo Reuters/AFP/

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW