1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona: Mawaziri wa Afya wa nchi za Umoja wa Ulaya wakutana

Zainab Aziz Mhariri:  Iddi Ssessanga
6 Machi 2020

Kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona kunaendelea kuwatia watu wasiwasi ulimwenguni kote. Mawaziri wa afya wa Umoja wa Ulaya wamekutana mjini Brussels kujadili njia za kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi hivyo.

Berlin Coronavirus - Pressekonferenz Gesundheitsminister
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Juhudi zinafanyika duniani kote kwa lengo la kukabiliana na dharura hiyo. Waziri wa afya wa Ujerumani Jens Spahn amesema virusi vya Corona vimeshaingia barani Ulaya na kwamba sasa pana changamoto ya kupunguza na kudhibiti kasi ya maambukizi yake. Waziri  Spahn ametamka hayo wakati mawaziri wa afya kutoka nchi nyingine 27 za Umoja wa Ulaya wakiwasili mjini Brussels kwa ajili ya mkutano huo. Hata hivyo ameeleza kuwa hakuna haja kwa Ujerumani kupunguza uhuru wa watu kuvuka mipaka kati ya nchi za Umoja wa Ulaya.

Italia, ambako takriban watu 148 wamekufa ni nchi ya Umoja wa Ulaya iliyoathirika zaidi kuliko nchi nyingine za jumuiya hiyo. Ufaransa imeripoti kuwa mtu wa tisa amefariki nchini humo baada kuambukizwa virusi vya COVID-19.

Waziri wa afya wa Ujerumani Jens SpahnPicha: picture-alliance/dpa/P- Zinken

Makao makuu ya kanisa katoliki Vatican yamethibitisha kisa cha kwanza cha virusi hivyo leo Ijumaa na kwamba imezifunga ofisi zake kadhaa kama hatua ya tahadhari wakati kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis akiendelea kupata nafuu baada ya kupata mafua. Kituo cha afya ndani ya Jiji la Vatican kimefungwa kwa ajili ya kukifanyia usafi.

Kwingineko dunaini hatua zinachukuliwa ili kuzuia kuenea kwa maambukizi. Mji wa Bethlehem umewekwa chini ya karantini baada ya mikasa ya Corona kubainika leo.

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet ametoa wito kwa serikali na wafanya biashara kusaidia kupunguza athari inayosababishwa na hatua za karantini pamoja na hatua zingine zinazolenga kupambana na mlipuko wa virusi vya Corona. Bachelet amesema hatua za kupambana na virusi hivyo lazima zizingatie haki za binadamu, na juhudi zifanyike za kuwalinda watu walio hatarini zaidi katika jamii.

Kwa mujibu wa taarifa Idadi ya watu walioambukizwa virusi vya Corona duniani kote imefikia 98,123 na waliokufa ni 3385 katika nchi 87. 

Vyanzo:/AFP/AP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW