1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona: Mwaka mmoja baada ya kutangazwa janga

11 Machi 2021

Leo Alhamisi, ulimwengu unaadhimisha mwaka mmoja tangu virusi vya corona vilipotangazwa kuwa janga la ulimwengu.

Schweiz Genf | WHO Direktor Tedros Adhanom Ghebreyesus
Picha: Martial Trettini/KEYSTONE/picture alliance

Na licha ya chanjo kuanza kutolewa, maisha bado hayajarudi kama kawaida kutokana na vikwazo mbalimbali vilivyowekwa ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa COVID-19. 

Machi 11 Siku kama ya leo, mwaka uliopita itasalia kuwa kumbukumbu ulimwenguni. Ndio siku ambayo Shirika la Afya Duniani, WHOlilipoutangaza rasmi ugonjwa wa COVID-19 kuwa janga la ulimwengu.

"Tumeingiwa na wasiwasi juu ya ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona na kiwango duni cha kutochukua hatua. Kwa hiyo tumefanya tathmini yetu na tumeamua kuutangaza ugonjwa wa Covid-19 kuwa janga la dunia." alisema Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Wakati huo, watu wapatao 4,600 walikuwa wamefariki kutokana na ugonjwa huo.

Soma zaidi: WHO: Hakuna dalili za corona kuisha mwaka huu

Uzito wa janga la virusi vya corona sasa unaingia mwaka wake wa pili tangu kutangazwa kuwa janga la ulimwengu.

Nchini Brazil kwa mfano, jana Jumatano watu 2,286 walifariki duniani kutokana na ugonjwa wa COVID-19 unaoshambulia zaidi mapafu. Katika siku za hivi karibuni, nchi hiyo ya Amerika ya Kusini imeshuhudia ongezeko la wagonjwa waliokutwa na virusi vya corona.

Corona iliathiri sio tu sekta ya afya, bali hata kuyumbusisha uchumi wa dunia

Picha: Hannah Beier/REUTERS

Sio tu sekta ya afya ilioathirika na Janga la COVID-19, bali pia uchumi wa ulimwengu. Bunge la Marekani limeupitisha mpango wa uokozi wa dola trilioni 1.9 kwa ajili ya kuufufua uchumi wa nchi hiyo. Rais Joe Biden amesema mpango huo utazisaidia familia zisizojiweza.

Wakati Marekani ilipoanza kuhisi athari za moja kwa moja za janga la COVID-19, Donald Trump aliyekuwa rais wakati huo alionekana kupuuza ugonjwa huo. Trump aliwambia Wamarekani na hapa namnukuu: "Hivi virusi vya corona havitakuwa na nafasi yoyote dhidi yetu."

Chini ya uongozi wake, Marekani ilikuwa nchi iliyoathirika zaidi na janga hilo na kwa wakati huu, idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa COVID-19 nchini humo ni zaidi ya 528,000.

Yumkini namna pekee ya kupambana na ueneaji wa virusi hivyo mwaka uliopita ilikuwa ni uvaaji wa barakoa na kuzuia watu kutengamana.

Umetimia mwaka mmoja tangu kisa cha kwanza cha corona kuthibitishwa Ujerumani

01:33

This browser does not support the video element.

Janga hilo liliisimamisha dunia: Usafiri wa anga ukazuiwa, serikali mbalimbali zikaweka vikwazo ikiwemo kuwazuiwa watu kusafiri au kutotoka nje kwa muda fulani, na hata kupiga marufuku shughuli za kiuchumi na masomo.

Hata hivyo, mwaka mmoja baadaye, watu wameanza kupata matumaini, ujasiri, na hata kuondoa uwoga uliokuwepo awali. Watu wameanza japo hatua kwa hatua kurudia maisha yao ya kawaida.

Leo hii, chanjo zimeanza kutolewa na kusambazwa katika kila pembe ya dunia. Kwa mujibu wa takwimu za shirika la AFP, zaidi ya dozi milioni 300 zimesambazwa kwa karibu nchi 140 duniani. Hakika, baada ya dhiki ni faraja.

Chanzo: Mashirika

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW