1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona: Shughuli zinaanza kurudi kama kawaida China

Babu Abdalla6 Machi 2020

Korea Kaskazini imesema imewaachia raia 220 wa kigeni waliokuwa wamewekwa kwenye karantini ilhali katika mkoa wa Hubei, China hakujaripotiwa visa vyovyote vya maambukizi mapya ya Corona katika muda wa zaidi ya saa 24.

Coronavirus in Südkorea Drive-Through-Test
Picha: AFP/Jung Yeon-je

Wageni 221 kati ya takriban 380 nchini Korea Kaskazini waliokuwa chini ya uangalizi wa madaktari wameruhiwa, chombo cha habari kinachomilikiwa na serikali kimetangaza. Chombo hicho hata hivyo hakikutoa maelezo zaidi.

Baadhi ya vyombo vya habari vya kigeni ikiwemo runinga inayosimamiwa na serikali ya Urusi vimeripoti kuwa baadhi ya wageni walioko Pyongyang huenda wakahamishwa hivi karibuni.

Korea Kaskazini imesema kuwa takriban watu 7,000 walikuwa chini ya uangalizi wa madaktari. Maafisa nchini humo wamesema kuwa wameongeza uchunguzi hasa kwa watu wanaoingia nchini humo kutoka mataifa yalioathirika na mlipuko wa Corona au watu walioingiliana na wageni.

Virusi vya COVID-19 vimekuwa vigumu kubainika, kuvidhibiti au hata kuvitibu huku wataalam wakiingiwa na wasiwasi juu ya mlipuko nchini Korea Kaskazini kuwa huenda ukasababisha madhara makubwa kufuatia ukosefu wa vifaa vya kisasa vya matibabu nchini humo.

Nchi hiyo iliyoko barani Asia imepiga marufuku watalii wa kigeni kuingia nchini humo, imefunga mipaka yake na pia imechelewesha ratiba yake ya shule. Kadhalika, imewahamasisha maelfu ya wafanyakazi wa serikali kuhusu mbinu za kujikinga dhidi ya virusi vya Corona.

Picha: picture-alliance/AP/Ahn Young-joon

Na nchini China katika jimbo la Hubei, ukiondoa mji wa Wuhan, hakuna visa vyovyote vipya vya maambukizi ya Corona vilivyoripotiwa kwa zaidi ya saa 24. Hio ni mara ya kwanza tangu kutokea kwa mlipuko wa virusi hivyo. Mamlaka nchini humo inaendela kufanya juhudi ili kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo katika maeneo mengine.

Hata hivyo katika mji wa Wu-han ambao ni kitovu cha mlipuko wa virusi vya Corona kumeripotiwa visa vipya 126 vya maambukizi ya Corona Alkhamisi, tume ya kitaifa ya afya imesema leo Ijumaa.

Licha ya visa hivyo vipya kuripotiwa, ishara zote zinaonyesha kuwa hali ya kawaida inaanza kurudi kama awali kwani tayari shule zimefunguliwa.

Kwengineko, waziri wa Afya wa Cameroon amethibitisha kisa cha kwanza cha virusi vya Corona nchini humo. Katika taarifa, wizaya ya afya imesema kuwa mgonjwa huyo, raia wa Ufaransa mwenye miaka 58 aliwasili katika mji mkuu wa Yaounde mnamo Februari 24.

Vyanzo Reuters, AP