1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona: Tanzania na Zanzibar zavunja kimya chao

Salma Said23 Februari 2021

Tangu wimbi la pili la Corona lilipoanza kuihangaisha dunia, Tanzania na Zanzibar zilikuwa kimya huku wasiwasi ukitanda hasa baada ya baadhi ya viongozi kufariki dunia na vifo hivyo kuhusishwa na ugonjwa wa Covid-19.

Tansania Dar es Salaam | Grafitty zu Corona
Picha: Eric Boniphace/DW

Baada ya kimya hicho hatimaye Serikali ya Zanzibar imetowa tamko la kuwataka wananchi kuchukuwa tahadhari kubwa dhidi ya maradhi mbalimbali ikiwemo tatizo la kupumuwa na virusi vya corona. Mwandishi wetu Salma Said ametuletea taarifa ifuatayo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera Uratibu na Baraza la Wawakilishi Dk. Khalid Salum Mohammed ametaka kila mmoja kuchukua tahadhari kwa ajili ya kuyalinda maisha yake.

"Tudumishe usafi wa mikono kwa kunawa mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au vitakasa mikono. Maeneo yote yanayotoa huduma kwa watu wengi ni vyema wahusika wakaweka sehemu na vifaa vya kunawia mikono kwa maji tiririka na sabuni au vitakasa mikono," amesema Dk. Khalid Salum Mohammed.

Katika siku za hivi karibuni Dk. Khalid amekiri kumejitokeza wananchi wengi ambao wanasumbuliwa na maradhi ya homa ya mapafu, homa kali na shida ya kupumua huku akiahidi kuwa serikali itafuatilia kwa karibu na kuchukua jitihada kubwa kupitia wataalamu wake ili kuidhibiti hali hiyo, na hapa anataja mambo muhimu za kuzingatia.

Rais Magufuli awataka wananchi kuacha kutumia barakoa zinazotoka nje ya nchi

Picha: Tanzania Presidents Office

Rais wa Tanzania, John Magufuli hivi karibuni aliwataka wananchi kuacha kutumia barakoa zinazotoka nje ya nchi kwa sababu baadhi yake sio salama. Hata hivyo, Serikali ya Zanzibar imekwepa kueleza waziwazi suala hilo, lakini imesisitiza kutumia barakoa zinazotengenezwa nchini. Dk. Khalid ameongeza:.

"Wakati wote tunapotoka nje ya nyumba zetu hasa tunapokuwa katika mikusanyiko na watu tuvae barakoa hasa zile zilizotengenezwa kwa vitambaa hapa hapa nchini. Aidha inasisitizwa barakoa hizo zifuliwe kwa maji na sabuni kabla ya kutumia tena. Tunapokohoa au kupiga chafya tufuate masharti ya kiafya ikiwemo kufunika mdomo kwa kutumia kitambaa safi au kiwiko cha mkono."

Sambamba na hilo serikali ya Zanzibar imewashauri wananchi kuendelea kutumia dawa za kiasili kwa ajili ya kinga na tiba ya maradhi hayo kama anavyoeleza zaidi Dk. Khalid:

"Kwa wale wenye dalili za kukohoa, mafua makali au shida ya kupumua tunatakiwa kuripoti Kituo cha Afya kilicho karibu ili kupata ushauri unaostahiki. Tuwe na utaratibu wa kula chakula bora ikiwemo matunda na mboga mboga pamoja na kufanya mazoezi."

Licha ya kutoa tahadhari kwa wananchi, serikali bado imesalia kimya kuhusu upimaji na utoaji wa takwimu za wagonjwa wa virusi vya corona baada kusitishwa zoezi hilo Aprili 2020. Tayari nchi za Uingereza na Oman zimewazuwia wasafiri kutoka Tanzania kuingia katika nchi hizo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW