Rais Trump ataka Wamarekani kuchukua tahadhari
1 Aprili 2020Ikulu ya White House inatabiri kuwa huenda idadi ya vifo vinavyotokana na virusi vya Corona ikawa kati ya watu 100,000 hadi 240,000 nchini Marekani hata iwapo miongozo iliyotolewa ya watu kukaa mbali na wenzao itazingatiwa.
Rais Donald Trump ametilia uzito tahadhari hiyo kwa kusema ni suala la kufa na kupona. Rais huyo amewataka Wamarekani kuzingatia maagizo yaliotolewa na maafisa wa afya ili kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.
Tayari zaidi ya Wamarekani 3,500 wamefariki kutokana na virusi hivyo huku wengine zaidi ya 170,000 wakiambukizwa virusi hivyo.
Na nchini Saudia Arabia, waziri anaehusika na masuala ya Hajji na Umrah ametoa wito kwa waumini wa dini ya Kiislamu wanaokusudia kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu kuchelewesha kupanga safari zao, katika ishara ya uwezekano wa kufutwa kwa ibada hiyo kutokana na hofu ya kuenea kwa virusi vya Corona.
Waislamu wanaokusudia kutekeleza ibada ya Hija washauriwa kuchelewesha kupanga safari zao
Mnamo mwezi Februari utawala wa kifalme nchini humo uliamua kuifunga miji mitakatifu ya Makka na Madina, hatua ambayo ililenga kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona. Miji hiyo haijawahi kufungwa hata wakati wa janga la homa ya mafua makali ya mwaka 1918 iliyojulikana kama Mafua ya Uhispania, ambayo iliwaua mamilioni ya watu kote duniani.
Nchi hiyo ya kifalme imeweka vizuizi kadhaa ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya Corona. Kwa sasa, Saudia Arabia imethibitisha zaidi ya maambukizi 1,500 ya virusi vya Corona na imerekodi vifo 10 kutokana na ugonjwa wa COVID-19.
Kwa ujumla eneo la Mashariki ya Kati limethibitisha zaidi ya visa 71,000 vya maambukizi ya virusi vya Corona huku Iran ikirikodi visa vingi zaidi.
Na nchini Afghanistan, baraza la Usalama la Umoja wa mataifa limezitolea wito pande zinazohasimiana nchini humo kuweka chini silaha na badala yake kushughulikia janga la COVID-19.
Naibu mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa Ingrid Hayden amesema nchi hiyo imefikia hatua muhimu ambayo inastahili viongozi wake wakae katika meza moja ya mazungumzo ili kuhakikisha amani inapatikana.
Na aliyekuwa Rais wa klabu ya mpira ya Marseille Pape Diouf amefariki dunia kutokana na virusi vya Corona akiwa na umri wa miaka 68.
Diouf alikuwa amelazwa katika hospitali moja nchini Senegal baada ya kuambukizwa virusi hivyo, na anakuwa mtu wa kwanza nchini humo kufariki kutokana na ugonjwa wa COVID-19.
Chanzo AP