Hawana vifaa vya kujikinga dhidi ya Corona
20 Machi 2020Mary Grace Aves ana hofu nyingi ya yeye na familia yake kuambukizwa na virusi vya Corona, lakini katika makazi yake yaliyoko kwenye mtaa wa mabanda wa Tondo haiwezekani kutelekeza mikakati ya kujinga dhidi ya virusi hivyo. Anasema ni vigumu kubakia nyumbani na pia hakuna usafi wa mazingira katika mtaa huo ulio karibu na mji mkuu wa Ufilipino, Manila.
Katika mtaa huo pia, Aves anasema kuna uhaba wa vifaa vya kujikinga dhidi ya virusi vya Corona kama barakoa na dawa ya maji ya kuuwa vijidudu.
Hofu yake inafanana na ya mamia ya mamilioni ya watu kama yeye wanaoishi mitaa ya mabanda katika bara la Asia ambapo kuna usafi duni wa mazingira na pia wakaazi wanapasa kutoka nyumbani kwenda kutafuta riziki ya kila siku.
Mataifa mengi ya bara Asia yametangaza mikakati mikali ya kupambana na kuenea kwa virusi vya Corona huku Ufilipino ikiamrisha nusu ya idadi ya watu wake wapatao milioni 110 kusalia majumbani.
''Katika mitaa yetu ya mabanda ni vigumu sana sisi kuwazuia watu kuingi ndani au kutoka, nina hofu kuna uwezekano sote tukaambukiziwa na virusi hivyo,'' Fely Tumbaga mkaazi wa mtaa wa Tondo amesema.
Wataalamu wa afya duniani wamesema kuwa kinga zaidi dhidi ya virusi hivyo ni kubakia nyumbani na kunawa mikono mara kwa mara ili kudhibiti ueneaji wa virusi hivyo vinavyosambaa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.
Kulingana na ripoti ya benki ya dunia ya mwaka 2017, maeneo ya mashariki mwa bara la Asia na eneo la Pasifiki yana takribani watu milioni 250 wanaoishi mitaa ya mabanda, wengi wao wakiwa China, Indonesia na Ufilipino. Ripoti hiyo aidha inasema kuwa watu hao hupika, hufua nguo na pia kuendeleza shughuli zao nyingine za maisha katika maeneo yaliyojazana, na hivyo basi ni lazima watu kuwa hadharani ili kuweza kuishi.
Nyumba za watu hao zimekaribiana sana kupita kiasi, bila maji safi na pia zina nafasi ndogo tu ya kulala, ripoti hiyo inaeleza.
Virusi vya Corona vikikizidi kuenea kwa kasi duniani, mataifa masikini zaidi ya bara la Asia yameachwa kujikinga kivyake dhidi ya virusi hivyo. Indonesia na India bado hazijaweka karantini kwenye miji yake.
Nchini Pakistan, waziri mkuu Imran Khan amesema serikali ya nchi hiyo haitofungia miji yake, akisema kuwa hatua hiyo itaathiri pakubwa uchumi wa taifa hilo.
Kufikia sasa, zaidi ya mambukizi 218,000 ya virusi vya Corona yameripotiwa ulimwenguni kote huku takribani watu 9,000 wakifariki kutokana na ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi hivyo vya Corona.
Chanzo : AFPE