1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona: Watu 1,641 wafariki siku moja Brazil

3 Machi 2021

Brazil imerekodi idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Covid-19 kwa siku baada ya watu 1,641 kufariki kwa ugonjwa huo.

Coronavirus | Brasilien Trauer um Covid-19-Opfer
Picha: Andre Coelho/Getty Images

Wakati huo huo Rais wa Marekani Joe Biden ameahidi kuwepo kwa chanjo ya kutosha itakayomfikia kila mtu nchini humo kufikia mwisho wa mwezi Mei.

Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya afya nchini Brazil, idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na vifo 1,595 vilivyotokea kwa siku moja mwishoni mwa mwezi Julai, mwaka 2020.

Nchi hiyo ya America ya Kusini yenye idadi ya watu milioni 212 inakabiliwa na wimbi jipya la maambukizo ya virusi vya Corona huku hospitali zikionekana kulemewa na idadi kubwa ya wagonjwa.

Zaidi ya watu 257,000 wamekufa kwa ugonjwa wa Covid-19 nchini humo na kuifanya nchi hiyo kuwa miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi na janga la virusi vya Corona baada ya Marekani.

Viongozi wa majimbo walisema jana Jumanne kuwa wataungana ili kununua chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 baada ya serikali kuu kuonekena kujikokota katika mpango wake wa utoaji chanjo.

Miji kadhaa tayari imeanza kuweka vikwazo vipya ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona.

Biden aahidi kuwepo chanjo ya kutosha Marekani

Picha: Jonathan Ernst/REUTERS

Nchini Marekani, Rais Joe Biden ameahidi kuwepo kwa chanjo ya kutosha nchini humo katika muda wa miezi michache ijayo. Akiwa mjini Washinton, Biden amesema atahakikisha mpango wa utoaji chanjo utamfikia kila mtu kufikia mwishoni mwa mwezi Mei.

Biden pia ametangaza kuwa waalimu wanapaswa kupewa kipau mbele kupokea chanjo hiyo, hatua ambayo itakuwa muhimu kuelekea kuanza tena kwa shughuli za masomo.

"Miongoni mwa vipau mbele vyangu vya kwanza nilipoingia ofisini, ni kuwa dozi milioni 100 za chanjo zitakuwa zimetolewa katika siku zangu 100 za kwanza ofisini. Tayari tumefika nusu ya idadi hiyo katika muda wa siku 37 na nina imani tutafanikiwa," amesema Biden.

Mnamo siku ya Jumamosi, Marekani iliidhinisha chanjo ya Johnson & Johnson na kuifanya chanjo hiyo kuwa ya tatu kuidhinishwa kwa ajili ya matumizi nchini humo. Chanjo zingine zilizoidhinishwa ni pamoja na Pfizer/BioNTech na Moderna.

Kwengineko, shehena ya Chanjo imezifikia mataifa ya Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Angola kupitia mpango wa kimataifa wa usambazaji chanjo,Covax.

Kupitia mpango huo, Nigeria imepokea dozi milioni nne, Jamhuri ya Kidemokrasia imepokea dozi milioni 1.7, Angola imepokea zaidi ya dozi 600,000 wakati Gambia ikitarajia kupokea kiasi dozi 30,000.

Wiki iliyopita, Ghana na Ivory Coast zilikuwa nchi za kwanza barani Afrika kupokea chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 kupitia mpango huo wa Covax, ambao unalenga kusamba dozi bilioni mbili kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW