1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona: Watu zaidi ya 600,000 waambukizwa duniani kote

Zainab Aziz Mhariri: Buwayhid, Yusra
28 Machi 2020

Idadi ya watu walioambukizwa ugonjwa wa homa ya mapafu COVID -19 unaosababishwa na virusi vya corona imeongezeka duniani kote.Hadi kufikia Jumamosi watu zaidi ya 600,000 walikua wameambukizwa.

Corona Symbolbild Europa Spanien
Picha: Getty Images/J. Soriano

Marekani sasa inaongoza ulimwenguni kwa idadi ya watu walioambukizwa ambao ni zaidi ya 104,000. Kulingana na takwimu zilizotolewa na chuo kikuu cha John Hopkins watu zaidi ya 607,000 wameambukizwa na zaidi vifo 28,000 vimetokea kutokana na ugonjwa wa COVID- 19. Chuo hicho kimeelezea kwamba kuna kazi nyingi bado inayopaswa kufanywa kwa ajili ya kupunguza kuenea kwa virusi vya corona.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ambaye amejitenga nyumbani baada ya daktari wake kupimwa na kupatikana kuwa ameambukizwa virusi vya corona, amesema sio rahisi kuzuia kabisa maambukizi katika hatua hii, lakini ni jambo la lazima katika siku za usoni kuweza kudhibiti kasi ya maambukizi ya virusi hivyo. Virusi vya corona tayari vimesabaisha matatizo makubwa katika mifumo ya afya nchini Italia, Uhispania na Ufaransa.

Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: AFP/M. Kappeler

Mkuu wa wafanyakazi katika ofisi ya Merkel, Helge Braun, amesema Ujerumani imechukua hatua ya kuyafunga maduka yasiyouza bidhaa zinazohitajika kwa maisha ya kila siku na kuweka marufuku ya mikusanyiko ya zaidi ya watu wawili na kwamba vizuizi hivyo havitaondolewa kabla ya tarehe 20, Aprili.

Wakati huo huo, ndege ya jeshi la Ujerumani leo Jumamosi imewasafirisha wagonjwa sita wanaougua ugonjwa wa COVID -19 kutoka mji wa kaskazini ya Italia wa Bergamo hadi mjini  Cologne, Ujerumani. Watu hao wamepelekwa katika hospitali mbali mbali nchini Ujerumani kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Mji wa Wuhan kulikoanzia mlipuko wa maambukizi ya corona ambako wanaishi takriban watu milioni 11 limeruhusu kuanza kufanyika shughuli za kila siku baada ya mji huio kuwekrewa marufuku na kulazimika kubakia majumbani kwa zaidi ya miezi miwili.

Na barani Ulaya wataalam wameelezea kwamba nchi kadhaa zitashuhudia ongezeko la watu wanaokufa kutokana na ugonjwa wa COVID -19 unaosababishwa na maambukizi ya virusi vya corona katika wiki zijazo. Italia na Uhispania zinakabiliwa na hali ngumu, maambukizi yanaongezeka kwa kasi na idadi ya watu wanaokufa pia inaongezeka kwa haraka kila uchao.

Vyanzo:/AP/ DW

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW