1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona yaiingiza Marekani na China kwenye vita vipya

17 Machi 2020

Mzozo mkali umeibuka hii leo kati ya China na Marekani kuhusiana na virusi vipya vya corona, baada ya rais Donald Trump kuighadhabisha Beijing kwa kuviita virusi hivyo kama "virusi vya China". 

US-Präsident Donald Trump
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Brandon

Mataifa hayo mawili kwa siku kadhaa sasa yamekuwa yakishambuliana kuhusu chanzo cha virusi hivyo vya corona, huku afisa mmoja wa China akituhumiwa kueneza nadharia za uwongo, akidai kwamba vililetwa nchini humo na jeshi la Marekani na maafisa wa Marekani wakitumia matamshi yanayoonekana yalilenga kuikandamiza China.  

Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter jana usiku kwamba "Marekani itayasaidia kwa kiasi kikubwa yale mashirika kama ya ndege na mengineyo, ambayo yameathirika sana na Virusi vya China." Matamshi yake yamekosolewa vikali ndani ya Marekani, huku kukitolewa onyo kwamba yanaweza kuchochea kisasi dhidi ya jamii yenye asili ya Asia na Marekani.

Washirika wa Trump huko nyuma walililitaja janga hilo kama "virusi vya corona vya China".

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya China, Geng Shuang ameonya kuhusu matamshi ya Marekani kuhusu virusi vya coronaPicha: picture-alliance/newscom/UPI/S. Shaver

Beijing imesema hii leo kwamba imekasirishwa sana na msemo huo ambao imeuita "aina fulani ya unyanyapaa". Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya China Geng Shuang amewaambia waandishi wa habari kwamba, Marekani inatakiwa kuacha mara moja madai yake ambayo haijayathibithisha dhidi ya China.

Vita hivyo vya maneno vimeibua wasiwasi wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili, ambayo yamekuwa katika mzozo wa kibiashara na mizozo mingine tangu rais Trumo alipoingia madarakani.

Wakati hayo yakiendelea, mkurugenzi mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, Tedros Adhanom Gebreyesus ametoa mwito kwa mataifa kuongeza kiwango cha upimaji kama njia bora zaidi ya kupunguza kusambaa kwa virusi vya corona. Gebreyesus alikuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, mapema hii leo.

"Lakini njia bora zaidi ya kuzuia maambukizo na kuokoa maisha na kukata minyororo ya maambukizi, na kufanya hivyo ni lazima kupima na kujitenga. Hauwezi kuzima moto wakati tumejifunika macho na hatuwezi kulizima janga hili ikiwa hatujui ambaye ameambukizwa. Tuna ujumbe rahisi kwa nchi zote: pima, pima, pima. Pima kila kisa kinachotiliwa shaka. " Amesema Gebreyesus.

Nchini Ujerumani, kutaanza kuchukuliwa hatua za kuwarejesha raia waliokwama mpakanai, wakati mipaka ikifungwa na mashirika ya ndege yakisitisha safari kutokana na janga la corona, hii ikiwa ni kulingana na waziri wa mambo ya nje Heiko Maas, katika wakati ambapo Berlin ikitoa onyo rasmi dhidi ya watu wanaotaka kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya likizo.

Serikali ya Ujerumani imekubali kutumia euro milioni 50, katika makubaliano iliyoingia na mashirika ya ndege ya kibiashara kuwarudisha raia hao nchini kwao. Kansela Angela Merkel, jana aliwaomba wajerumani wote kusitisha likizo na kutangaza hatua pana za kuwazuia nyumbani ili kukabiliana na kusambaa zaidi kwa virusi hivyo.

Soma zaidi: WHO: Dunia imeingia hali ya mashaka kufuatia virusi vya Corona

Mashirika: AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW