Corona yazua hofu katika bunge la Kenya
8 Aprili 2020Vikao hivyo maalum vilivyokuwa vifanyike Jumatano vimeahirishwa kwa hofu ya maambukizi miongoni mwa wajumbe wengine.
Zaidi ya wajumbe 200 ambao wamepimwa virusi vya Corona, wakiwemo maspika wa bunge la seneti na la taifa wanaendelea kupokea matokeo ya vipimo vyao kutoka kwa Wizara ya Afya. Kikao maalum cha mabunge hayo kilisitishwa ghafla na maspika ambao wamekanusha madai ya kuwa wajumbe ni wagonjwa.
Spika wa Seneti Kenneth Lusaka amesema kuwa vikao hivyo vilisitishwa kwa kuzingatia agizo la Rais Uhuru Kenyatta la kukomesha safari za kuingia na kutoka jijini Nairobi ifikapo saa moja usiku kwa siku 21 zijazo. Hata hivyo shughuli jijini Nairobi zinaendelea kama kawaida isipokuwa tu kuanzia mwendo wa saa moja usiku.
Baadhi ya wajumbe walitangamana na wat waliopatikana na virusi vya corona
Duru zinaeleza kuwa hatua hiyo ilitokana na ujio wa baadhi ya wajumbe kutoka kwenye mataifa yaliyokuwa yameshambuliwa na virusi hivyo. Katika kikao cha seneti kilichopita, seneta Kipchumba Murkomen alidai kuwa baadhi ya wajumbe walikuwa wametangamana na watu waliodhaniwa kuwa na ugonjwa huo akiwemo naibu gavana wa Kilifi Gedion Saburi aliyepatikana na ugonjwa huo, lakini akapona baada ya matibabu.
"Tunahitaji kuchukua likizo ya mwezi mzima, tunapoweka mikakati, itakayotuwezesha kukabiliana na changamoto na jinsi ya kuhusiana tutakaporudi,” alisema Kipchumba Murkomen.
Juma lililopita, baadhi ya wajumbe na wafanyikazi wa bunge walilazimika kujitenga kwa kipindi cha siku 14 kutokana na kukaribiana na baadhi ya wabunge waliorejea nchini. Kiongozi wa kambi ya upinzani katika bunge la Taifa John Mbadi amesema kuwa hatua iliyochukuliwa inalenga kuwapa wabunge nafasi ya kupimwa na kupata matokeo ya vipimo vile. Hata hivyo Karani wa Bunge la Taifa Michael Sialai amethibitisha kuwa bunge litaendelea na vikao vyake Jumanne ijayo.
Kituo cha kuwapima wabunge kimejengwa
Tume ya huduma za Bunge imejenga kituo cha kuwachunguza na kuwapima wajumbe pamoja na wafanyikazi wanaohudumu humo. Hayo yanajiri huku, serikali ikiweka sheria kali kwa wale wanaokiuka maagizo ya kujitenga iwapo wamekaribiana na wagonjwa wa covid-19 ama wameonesha dalili zake. Mutahi Kagwe ni Waziri wa Afya.
"Mtu yeyote atakayekiuka sheria ya kujitenga atalazimishwa kuwekwa kwenye karantini, kwa siku 14, kisha baadaye atiwe nguvuni na ashtakiwe,” alisema Mutahi Kagwe.
Ripoti zinaonesha kuwa zaidi ya wabunge 50 na wafanyikazi wa bunge walitangamana na mbunge wa Rabai Kamoti Mwamkale, ambaye alipatikana na ugonjwa wa covid-19. Hofu iliyoko pia ni kwa waandishi habari ambao wamekuwa wakitangamana na wabunge hao kwenye vikao vya bunge. Watu 2000 wamewekwa karantini katika vituo mbali mbali kote nchini, huku wengine 5000 wakipimwa, kufikia sasa.