1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Costa aitaka Iran kusitisha mashambulizi Mashariki ya Kati

31 Machi 2026

Rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa amemtaka Rais wa Iran Masoud Pezeshkian kusitisha mashambulizi katika eneo la Mashariki ya Kati.

Ubelgiji Brussel 2025 | António Costa bei Pressekonferenz nach EU-Gipfel
Rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa akiwa katika kikao na waandishi wa habari mnamo Desemba 19, 2025Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Baada ya mazungumzo ya simu na Masoud Pezeshkian, Antonio Costa amesema amesisitiza haja ya kupunguza makali ya mapigano, kulinda raia na miundombinu ya kiraia, pamoja na pande zote kuheshimu sheria za kimataifa.

Ameitaka  Iran kusitisha mashambulizi aliyoyaita yasiyokubalika dhidi ya mataifa ya kanda na kujihusisha kikamilifu katika juhudi za kidiplomasia.

Costa ameongeza kuwa hatua hiyo pia inahusisha kushirikiana na Umoja wa Mataifa ili kuhakikisha uhuru wa usafirishaji katika Mlango-Bahari wa Hormuz, akisisitiza kuwa lazima kuwe na nafasi ya diplomasia.

Hegseth asema uwezo wa Iran unapungua

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth amesema mashambulizi ya Marekani yanaendelea kuipa Marekani nguvu zaidi katika uwanja wa vita huku uwezo wa Iran ukipungua.

"Hii ni kuhusu urithi. Mafanikio ni muhimu. Na kwa sababu ya rais huyu na Wamarekani hawa, tunakaribia ushindi zaidi kuliko hapo awali. Rais Trump anafanya kile ambacho hakuna rais mwingine aliyekuwa na ujasiri wa kukifanya. Marais waliopita walikuwa wa maneno, lakini yeye ni wa vitendo. Katika uwanja wa vita, kutokana na uhuru aliotupa, nguvu ya mashambulizi ya Marekani inaongezeka. Sisi tuna chaguo nyingi zaidi, wao wana chache.”

Rais wa Marekani Donald Trump Picha: Nathan Howard/REUTERS

Trump azitaka nchi zilizojitenga na vita Iran kujitegemea

Rais Donald Trump amezitaka nchi ambazo hazikushiriki katika mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran kununua mafuta kutoka Marekani au kwenda katika Mlango-Bahari wa Hormuz na "kuyachukua.”

Kupitia mtandao wake wa Truth Social, Trump aliitaja Uingereza kuwa miongoni mwa nchi ambazo hazikushiriki, akizitaka kujitegemea na kuongeza kuwa Marekani haitakuwa tayari tena kusaidia kama ilivyokuwa awali.

Qatar yasema mataifa ya Ghuba yana msimamo mmoja 

Qatar imesema mataifa ya Ghuba yana msimamo mmoja wa kutaka kupunguzwa kwa mapigano na kumalizika kwa vita vya Mashariki ya Kati, wakati Iran ikiendelea na mashambulizi mapya dhidi ya majirani zake.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Majed al-Ansari, amesema kuna umoja mkubwa katika kanda hiyo wa kuhimiza kupungua kwa mvutano na kusitishwa kwa vita.

Saudi Arabia yaokoa meli ya mafuta ya Kuwait

Mamlaka nchini Saudi Arabia zimesema meli ya mafuta ya Kuwait iliyoshambuliwa imeokolewa salama bila kuripotiwa kwa majeruhi wala uvujaji wa mafuta. Mapema, ofisi ya habari ya Dubai ilisema droni ililenga meli hiyo katika eneo la maji la Dubai.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW