Cote d'Ivoire, Cape Verde zaingia robo fainali AFCON
30 Januari 2024Wiki moja iliyopita ilionekana kana kwamba Wacote d'Ivoire wangefungasha virago katika hatua ya makundi katika AFCON inayoandaliwa nchini mwao, lakini sasa wametinga robo fainali baada ya kuwabwaga Senegel kwa penalti 5 kwa 4. Mechi ilikamilika kwa sare ya 1 -1 baada ya muda wa ziada.
Soma pia: Kongo, Guinea zatinga robo fainali ya AFCON
Tembo hao walipenyeza katika hatua ya mtoano na rekodi mbovu ya timu nne bora zilizomaliza katika nafasi ya tatu kwenye makundi, baada ya kukamilisha duru ya kwanza na kichapo cha fedheha cha 4 – 0 kwa Guinea ya Ikweta, ikiwa ni kichapo Kizito kabisa kuwahi kuwakumba katika ardhi ya nyumbani. Ilibidi wamtimue kocha mkongwe wa Kifaransa Jean-Louis Gasse na kujaribu bila mafanikio kumleta kocha wa zamani Herve Renard kwa mkopo.
Badala yake, mchezaji wa zamani Emerse Fae aliteuliwa kwa mkataba wa muda, na matumaini ya kuiamsha timu iliyokuwa imepigwa na butwaa kwa kibarua kikali dhidi ya mabingwa watetezi. "Ukizingatia tunakotoka, kufungwa bao la mapema kungetuzamisha. Wachezaji wangu walipambana vizuri,” alisema Fae.
Soma pia: Magoli 2 ya Lookman dhidi ya Kamerun yaipeleka Nigeria robo fainali
Ni kweli kwa sababu ilionekana ungekuwa usiku mrefu kwao wakati Habib Diallo alisukuma wavuni kombora katika dakika ya nne akiunganisha krosi ya Sadio Mane. Mane alinusurika na kadi ya njano kwa kumchezea rafu Ibrahim Sangare. Katika kipindi cha pili, Ismaila Sarr wa Senegal alianguka katika kijisanduku baada ya miguu yake kugongana na ya Odilon Kossounou, lakini hakuna penalti iliyotolewa. Wacote d'Ivoire kisha wakapata penalti baada ya VAR kuonesha Nicolas Pepe aliangushwa na kipa wa Senegal Edouard Mendy. Frank Kessie anayechezea Al Ahli ya Saudia alifunga mkwaju huo na kulazimisha mechi kuingia muda wa nyongeza. Ikawa ni wakati wa matuta kuamua, na Moussa Niakhate wa Senegal ndiye mchezaji pekee aliyepoteza penalti kwa kugonga chuma. Kessie kisha akafunga penalti ya mwisho na ya ushindi.
Soma pia: AFCON. Ghana yamtimuwa kocha timu ya taifa
Cote d'Ivoire sasa watacheza robo fainali dhidi ya Mali au Burkina Faso katika mji wa Bouake Jumamosi. Majirani hao wawili Mali na Burkina Faso wataangushana leo katika hatua ya 16 za mwisho kwenye mji wa kaskazini wa Korhogo. Mshambuliaji wa Cote d'Ivoire Sebastian Haller amesema baada ya mechi kuwa wamejawa na hisia nyingi. "Siku chache zilizopita hazijawa rahisi lakini ilitubidi tujiamini.”
Senegal inaondolewa baada ya kuwa timu pekee iliyoshinda mechi zote tatu katika hatua ya makundi, na kuondolewa kwao kuna maana hakuna bingwa mtetezi aliyewahi Kwenda mbali ya hatua ya kwanza ya mtoano ya AFCON tangu Misri iliposhinda taji la tatu mfululizo mwaka wa 2010.
Hadithi ya Cape Verde yaendelea kunoga
Mapema jana, Cape Verde ilishinda mechi ya hatua ya mtoano ya AFCON kwa mara ya kwanza katika historia yao baada ya penalti ya Ryan Mendes kuwapa ushindi wa 1 – 0 dhidi ya Mauritania mjini Abidjan.
Mechi hiyo ilikuwa inaelekea katika muda wa ziada wakati Cape Verde ilipata mkwaju wa penalti wakati mchezaji aliengia kutokea mbao ndefu Gilson Tavares Benchimol aliangushwa katika eneo hatari na kipa wa Mauritania Babacar Niasse. Nahodha Mendes kisha akasukuma wavuni mkwaju huo zikiwa tu zimesalia dakika mbili mchezo kuisha na kuivunja ngome ya Mauritania ambayo ilikuwa inashiriki hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza.
Cape verde wanatinga robo fainali watakayocheza Jumamosi mjini Yamoussoukro dhidi ya Morocco au Afrika Kusini, watakaokutana leo katika hatua ya 16 za mwisho mjini San-Pedro.
Taifa hilo dogo la kisiwa lilikuwa limefuzu hatua ya makundi katika mashindano mawili kati ya matatu waliyoshiriki ya AFCON, lakini hawakuwa wamewahi kushinda mechi ya mtoano. "tunajivunia kila kitu tulichofanya mpaka sasa. Kila mara sisi hujaribu kushinda mechi na tulistahili sana ushindi wa leo,” alisema kocha wa Cape Verde Pedro Bubista Brito, anayeamini kuwa timu yake inaweza kusonga mbele hata zaidi katika mashindano haya. Anasema lengo lao kuanzia siku ya kwanza lilikuwa ni kutinga nusu fainali na wanaamini wanaelekea huko.