1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COVID-19: Asia yahofia wimbi la pili la maambukizi

Daniel Gakuba
10 Mei 2020

Visa vipya vya maambukizi ya virusi vya corona vimejitokeza nchini China, Korea Kusini na Iran, hali inayotishia mafanikio yaliyopatikana dhidi ya virusi hivyo. Ujerumani nako kasi ya maambukizi imepanda tena.

China Wuhan | Hubei verringert die Corona-Alarmstufe
Picha: Getty Images/AFP/Str.

Wakati idadi jumla ya watu walioambukizwa virusi vya Corona duniani kote ikipindukia milioni nne (4,000,000) mji wa Wuhan nchini China ulikoanzia mripuko huo kumeripotiwa kisa kipya kwa mara ya kwanza katika muda wa zaidi ya mwezi mzima. Wimbi jipya linaloonekana katika nchi za Asia linaaminika kuwa na chimbuko katika vilabu vya usiku vya nchini Korea Kusini.

Leo Jumapili, Korea Kusini imethibitisha visa vipya 34, idadi hiyo ikiwa kubwa zaidi kusajiliwa kwa siku moja kwa zaidi ya mwezi mzima.

Ijumaa iliyopita wahudumu wa afya walifanya juu chini kutafuta watu waliowasiliana na kijana wa miaka 29 aliyethibitika kuwa na virusi vya corona, ambaye anaripotiwa kuvitembelea vilabu vitatu vya usiku katika kitongoji cha Itaewon chenye shughuli nyingi za burudani katika mji mkuu, Seoul.

Kitongoji cha Itaewon mjini Seoul kinachohofiwa kuwa chimbuko la wimbi jipyaPicha: Reuters/Yonhap News Agency

Kwa siku kumi mfululizo Korea Kusini imekuwa ikiripoti visa vichache kabisa vya COVID-19 kwenye ardhi yake.

Nchini China virusi vyaenea tena

Hapo jana nchini China visa vipya 14 vilithibitishwa, vikiwa vingi zaidi kwa siku moja tangu Aprili 28, na likiwa ongezeko la kisa kimoja zaidi ikilinganishwa na siku iliyotangulia. Kati ya visa vya jana, viwili ni miongoni mwa watu waliotoka nje ya nchi. Aidha, visa 11 kati ya vile vilivyotokana na maambukizi ya ndani vilikuwa katika mji wa Shulan ulio kwenye jimbo la Jilin kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo.

Wakati huo huo, nchini India mripuko mkubwa wa virusi vya corona umeonekana miongoni mwa maafisa wa polisi. Katika jimbo la Maharashtra pekee yake, ilibainika leo Jumapili kuwa maafisa wapatao 786 walikuwa wamepatwa na ugonjwa unaosababishwa na virusi hivyo. Jimbo hilo lililo magharibi mwa India linayo asilimia 30 ya visa jumla 63,000 vilivyokwishathibitishwa nchini humo hadi leo.

Maafisa wa polisi nchini India wanaandamwa na maambukizi ya coronaPicha: DW/M. Kumar

Nje ya jimbo hilo, maafisa wa polisi zaidi ya 70 wamethibitika kuambukizwa COVID-19 katika mji mkuu, New Delhi, na mmoja kati yao amekwishaaga dunia.

Kasi ya maambukizi yaongezeka Ujerumani baada ya kulegeza masharti

Huku hayo yakiarifiwa, nchini Ujerumani kasi ya maambukizi iliyokuwa imepungua imeanza kupanda tena, baada ya serikali kulegeza masharti ya kuwataka watu kubaki ndani ya nyumba zao.

Taasisi inayoratibu mapambano dhidi ya janga la corona ya Robert Koch imesajili visa vipya 667 na kufikisha idadi jumla ya waliopatikana na virusi hivyo nchini humo kufika 169,218. Kitovu kipya cha maambukizi hayo ni mji mdogo wa Coesfeld ulio mpakani na Uholanzi, ambako wafanyakazi 205 wa kiwanda cha kusindika nyama wameambukizwa.

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson anatarajiwa baadaye leo kuzindua mpango utakaokuwa ukionya kuhusu kiwango cha kitisho cha  virusi vya corona mithili ya ule unaotumiwa kutoa tahadhari juu ya kitisho cha ugaidi.

 

dvv/aw (AFP, AP, Reuters, dpa)

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW