1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COVID-19 imeathiri juhudi za kupambana na Malaria

Shisia Wasilwa
29 Septemba 2021

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ameihimiza jamii ya kimataifa kusimama imara katika vita dhidi ya malaria licha ya changamoto ya sasa ya janga la Covid-19, linaloukumba ulimwengu.

Kenia Uhuru Kenyatta
Picha: imago/i Images

Kenyatta ambaye pia ni Mwenyekiti wa sasa wa Muungano wa Viongozi wa Bara la Afrika dhidi ya Malaria (ALMA), amesema inasikitisha kwamba janga la Covid-19, limehujumu juhudi zote za kusaidia kukabiliana na Malaria.

Wito wa Rais Kenyatta unajiri wakati jitihada zote ulimwenguni, zikielekezwa kukabiliana na virusi vya corona, licha ya kuwa vifo vingi barani Afrika husababishwa na ugonjwa wa Malaria. Ripoti za mwaka 2019, zinaonesha kuwa Afrika iliorodhesha asilimia 94 kati ya watu waliopata malaria ulimwenguni.Watafiti wagundua aina sugu ya malaria barani Afrika

Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi alipohutubia kwa njia ya video Baraza la Kuangamiza Malaria, Rais Kenyatta amesisitiza haja ya kuzingatia ajenda ya ALMA yenye ajenda nne, muhimu zaidi ikiwa kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali na kitovu cha takwimu na kubadilishana mafanikio ya vita dhidi ya malaria katika kila nchi.  

"Tunahitaji kuhakikisha, kuwa tunahifadhi miundo msingi ambayo tulitengeza kwa ajili ya ugonjwa wa malaria. Ni muhimu kuwafahamisha washirika wetu kuwa vita dhidi ya Malaria ni muhimu.”

Kitovu hicho cha takwimu kimetumiwa na nchi kuchapisha mafanikio yao, huku nchi 10 ikiwemo Kenya, Rwanda na Ghana tayari zikibadilishana mafanikio yao kupitia majukwaa ya mitandao ya intaneti. ALMA imeshirikisha Jumuiya za Kiuchumi za kanda pamoja na viongozi wa Nchi na Serikali kwa lengo la kushughulikia changamoto kuu na kutoa suluhisho katika vita dhidi ya malaria. Takwimu nchini Kenya, zinaonesha kuwa takriban visa milioni 3.5 vya malaria huripotiwa kila mwaka katika vituo vya afya, huku vifo 10700 vikiandikishwa kwa mwaka. Daktari Peter Wasike anafafanua.

Bill Gates na aliyekuwa mke wake Melinda Gates ambao walianzisha wakfu wa mapambano ya MalariaPicha: Jon Hrusa/dpa/picture-alliance

"Sehemu za nyanda za juu kama bonde la ufa na magharibi, hushuhudia vifo vingi, watoto wa kati ya miaka minne hadi 14 hufa, hiyo ni asilimia 20, watoto wa miezi sita hadi miaka minne pia hufa hiyo ni asilimia 20 pia kwa mwaka.”

Kwa misingi hiyo, Rais alisema Kenya imewahusisha vijana kupitia mpango wa ‘kazi mtaani' ambao umewawezesha kuondoa uchafu katika maeneo yao na kusaidia kupunguza maradhi yanayosababishwa na maji ikiwemo pia malaria katika jamii zao. 

Wanachama hao wa Baraza la Kumaliza Malaria waliafikiana kuhusu haja ya kuboresha mifumo ya afya ya kijamii kama sehemu ya kupiga jeki juhudi za kukabiliana na malaria Barani Afrika. Mkutano huo uliohudhuriwa na wanachama wa Baraza la kumaliza Malaria kote ulimwenguni akiwemo aliyekuwa Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf, aliyekuwa Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, Bill Gates, Afisa Mkuu wa kundi la Dangote, Aliko Dangote pamoja na Balozi wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) anayehusika na mikakati na ufadhili wa afya ulimwenguni Ray Chambers.