COVID-19: Mgogoro mkubwa wanukia nchini Afghanistan
16 Juni 2021Wataalam wa afya wanasema hali mbaya ya ugonjwa wa COVID-19 inaweza kushindwa kudhibitiwa nchini Afghanistan. Madaktari wamesema idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona nchini humo imeongezeka kwa kasi katika muda wa wiki chache zilizopita, huku hospitali zikijitahidi kulishughulikia wimbi hilo la maambukizi yanayoongezeka kila uchao.
Maafisa wa afya karibu katika majimbo yote ya Afghanistan wanapaza sauti, wakisema nchi hiyo inakabiliwa na hali mbaya ya kiafya.
Madaktari katika hospitali kuu ya mjini Kabul wameiambia DW kwamba hakuna vitanda vya kutosha kwa ajili ya wagonjwa wapya wa COVID-19.
Tariq Akbari, mkuu wa Hospitali ya Afghan/Japan ameeleza kuwa wanavyo vitanda 150 lakini wamepokea wagonjwa 170 na pia wanakabiliwa na uhaba wa mitungi ya oksijeni ya kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji.
Mgogoro wa kiafya
Kulingana na Wizara ya Afya ya Afghanistan, zaidi ya watu 3,800 wameshakufa kutokana na ugonjwa wa COVID-19 hadi kufikia Juni 16, lakini wataalam wanasema idadi halisi huenda ikawa ni kubwa zaidi kwa sababu ya kiwango kidogo cha upimaji wa virusi vya corona, pia kutokana na kutosajiliwa vifo vingi vinavyotokana na ugonjwa wa COVID- 19.
Serikali imeagiza kufungwa shule, vyuo vikuu, kumbi na saluni ili kupunguza kasi ya kuenea maambukizi. Lakini hatua hizi hazijafaulu kudhibiti maambukizi kwa sasa, kwa sababu maeneo mengine ambayo virusi vinaweza kuenea kwa haraka kama masoko na maduka yako wazi kwa umma. Wakati huo huo watu wengi hawavai barakoa na hawazingatii tahadhari za kiafya na serikali haijatangaza mwongozo wa lazima utakaofuatwa na watu wote.
Kiwango cha watu waliopatiwa chanjo pia ni cha chini sana nchini Afghanistan. Nchi hiyo iliyo na takriban watu milioni 36 imewapatia chanjo watu milioni 1 tu. Chanjo imetolewa haswa kwa wafanyikazi wanaotoa huduma za afya na wa vikosi vya usalama. Wiki iliyopita, Afghanistan ilipokea dozi 700,000 za chanjo ya Sinopharm kutoka China.
Vyombo vya habari kimya kuhusu maambukizi yanayoogezeka
Ingawa mgogoro mkubwa wa kiafya unajitokeza nchini Afghanistan, vyombo vya habari havitoi kipaumbele kwa suala hili kimataifa. Waafghanistan, hata hivyo, wanaendelea kuchapisha picha na video za wagonjwa wanaougua COVID-19 kwenye mitandao ya kijamii, kuonyesha hali ilivyo mbaya nchini mwao.
Umasikini uliokithiri na miundombinu dhaifu ya afya ya umma ni kikwazo kikubwa katika vita vya kupambana na janga hilo nchini Afghanistan. Mzozo unaoendelea kati ya serikali na wanamgambo wa Taliban pia unachangia ugumu wa kushughulikia dharura za kiafya na hivyo nchi hiyo inarudi nyuma katika kulidhibiti janga la maambukizi ya virusi vya corona. Zaidi ya nusu ya wilaya za nchini Afghanistan ziko chini ya udhibiti wa kundi la Taliban, hivyo hakuna zoezi lolote la kuwapima watu linalofanyika katika maeneo hayo.
Wataalam wanasema Afghanistan inahitaji msaada wa haraka wa kimataifa ili kukabiliana na maambukizi ya virusi vipya vya corona "Delta", vinginevyo itashindikana kudhibiti hali nchini humo.
Chanzo:https://p.dw.com/p/3v2Md