1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

Covid-19: Visa vya dhulma vyaongezeka Mombasa

Faiz Musa5 Juni 2020

Visa 291 vya ukiukaji wa haki za binadamu vimerikodiwa katika Pwani ya Kenya tangu kuanza kutekelezwa kwa sheria za kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya corona miezi mitatu sasa.

Kenia | Menschenrechte | John Elungata
Kamishna wa kanda ya Pwani John Elungata akihutubia vyombo vya habari baada ya kupokea ripoti ya hali ya haki za binadamu katika kanda ya pwani ya Kenya, mjini Mombaa, Juni 5, 2020.Picha: DW/F. Musa

Katika ripoti ya pamoja ya mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu yakiongozwa na shirika la Haki Afrika, kaunti ya Mombasa inatajwa kuongoza kwa visa vya watu kushambuliwa na hata kuuawa ambapo inaripotiwa watu 103 wamevunjiwa haki zao, ikifuatwa na 52 katika kaunti ya Kwale na Taita Taveta ikiwa na visa 48.

Mashirika hayo sasa yanamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuondoa marufuku ya kutoka nje usiku na sheria nyengine ambazo zimechangia ukiukaji wa haki za binadamu. Hussein Khalid, mkurugenzi wa shirika la Haki Afrika, ameitaka serikali kuondoa mara moja amri ya kutotembea usiku.

"Hii hali iliyoko hivi sasa imechangia pakubwa katika kudhuru uchumi wa wananchi watu wengi hivi sasa umasikini umezidiwatu wamepoteza kazi zaidi na watu wanaishi katika hali ngumu kabisa," alisema Hussein Khalid.

Katika picha hii ya Machi 27, 2020, polisi wanaonekana wakiwalaazimisha abiria wa feri kulala kifudifudi baada ya kuwafyatulia gesi ya kutoa machozi na kuwatia mbaroni.Picha: picture-alliance/AP Photo

Ripoti hiyo inaonyesha kwamba miongoni mwa watu 20 waliouawa, watano wameuawa na maafisa wa polisi hasa wakati wa usiku. Vilevile visa vya dhuluma za kijinsia vimeripotiwa zaidi katika kaunti ya Kilifi ambapo mojawapo ya visa hivyo ni mtoto mwenye umri wa miaka minane kubakwa na kuuawa.

Naila Abdallah, kiongozi wa kundi la kutetea haki za watoto na wanawake amesema tangu Machi 13, visa vya dhuluma dhidi ya wanawake na watoto vimeongezeka pakubwa, ambapo watoto watatu waliuawa, akiwemo mmoja ambaye alikuwa bado hajazaliwa, baada ya mama yake kupigwa risasi.

Mkuu wa Polisi katika Pwani ya Kenya, Rashid Yaqub na Mratibu wa kanda ya Pwani, John Elungata wameipokea ripoti hiyo huku Elungata akithibitisha kupata ripoti za ukiukaji wa haki za binadamu na kusema uchunguzi unaendelea.

Idara inayosimamia utendaji kazi wa polisi maarufu kama IPOA, imesema wataifanyia utafiti ripoti hiyo na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya maafisa wa polisi watakaopatikana na hatia.

Mwandishi: Faiz Musa, DW/Mombasa

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW