1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

Covid-19: Wazee Uhispania watekelezwa vituoni

24 Machi 2020

Wanajeshi wa Uhispania waliopelekwa kupambana na virusi vya Corona wamebaini wagonjwa wazee waliotelekezwa na wengine wamekufa kwenye makaazi ya wazee. Vifo kadhaa vimeripotiwa kwenye makazi ya wazee nchini humo.

Spanien Katalonien Unabhängigkeits-
Referendum Poilzei schreitet ein
Picha: Getty Images/D. Ramos

Hayo yanatokea wakati Uhispania imebadili uwanja wa mchezo wa kuteleza kwenye barafu kuwa eneo la muda la kuhifadhi maiti kukabiliana na wimbi la vifo vinavyotokana na virusi vya Corona.

Taarifa kuhusu kugunduliwa wazee waliotelekezwa na wengine kupoteza maisha zimepatikana wakati wanajeshi walipokuwa wakiendelea na kazi ya kupuliza dawa kwenye nyumba nchini Uhispania.


Vifo kadhaa kutokana na ugonjwa wa COVID-19 vimerikodiwa kwenye makaazi ya wazee chungu nzima yaliyomo nchini Uhispania.


"Tutakuwa wakali na tusiotabirika tunaposhughulikia jinsi wazee wanavyotendewa kwenye makaazi haya" amesema waziri wa ulinzi wa Uhispania Margarita Robles wakati wa mahojiano na kituo binafsi cha televisheni cha Telecinco.


Ameongeza kuwa jeshi wakati wa utekelezaji majukumu waliyopewa wamewakuta baadhi ya wazee wakiwa wametelekezwa na wengine wakiwa wamekufa kwenye vitanda vyao. Uchunguzi tayari umeanzishwa kuhusiana na kadhia hiyo.

Wfanyakazi wa afya wakiandaa mazingira ya kuwasili kwa wagonjwa katika hospitali ya muda iliyotengenezwa kwa ajili ya wagonjwa wa covid-19. Wazee wengi zaidi ndiyo wamekuwa wahanga wa janga hilo.Picha: AFP/COMUNIDAD DE MADRID


Wakati hayo yanajiri, vifo vilivyotokana na virusi vya Corona nchini Uhispani vimepanda kwa kasi na kufikia watu 2,182 siku ya Jumatatu baada ya watu 462 kufariki dunia katika muda wa saa 24.


Taarifa hizo ni kulingana na takwimu za wizara ya afya nchini humo.


Wakati huo huo, uwanja wa ndani wa mchezo wa kuteleza kwenye barafu uitwao Palacio de Hielo uliopo kati kati ya mji mkuu Madrid umegeuzwa kuwa chumba cha muda cha kuhifadhi maiti.


Serikali ya jimbo uliko mji wa Madrid imesema uwanja huo utaanza kutumika ndani ya uda mfupi unaokuja.


"Hii ni hatua ya muda na isiyo ya kawaida inayolenga kupunguza maumivu kwa wanafamilia wa wahanga na hali ambayo hospitali ya mjini Madrid inakabiliana nayo" imesema sehemu ya taarifa ya serikali ya jimbo.


Hapo kabla msemaji wa ofisi ya mji amesema makaburi 14 yaliyopo mjini Madrid yatasitisha kupokea miili ya watu kwa sababu wafanyakazi wake hawana vifaa vya kujikinga na maambukizi ya Corona.

Uhispania ni nchi ya tatu kwa kuwa na idadi kubwa ya vifo vya covid-19, baada ya Italia na China.Picha: AFP/COMUNIDAD DE MADRID


Hatua iliyochukuliwa ni kubadili ukumbi wa mikutano ulio karibu kuwa hospital ya kuwatibu wagonjwa wa virusi vya Corona yenye uwezo wa kuchukua vitanda 5,500.


Wazee ndiyo kundi lililo kwenye hatari zaidi kwenye mlipuko wa janga la Corona linalotishia ulimwengu na maafisa kote duniani wametoa wito wa kuchukulia hatua kali kuwalinda.


Waziri wa Afya wa Uhispania Salvador Illa amewaambia waandishi habari kuwa makaazi ya wazee ni "kipaumbele cha ksingi cha serikali"

Illa ameongeza kusema "Tutaongeza ufuatiliaji mpana wa vituo hivyo"


Chini ya miongozo ya kupambana na virusi vya Corona, wafanyakazi wa afya wanatakiwa kuiacha miili ya watu walioshukiwa kufa kwa ugonjwa wa COVID-19 hadi pale daktari atakapowasili. Lakini kutokana na wimbi la vifo vinavyoendelea muda wa kusubiri unaweza kuwa mrefu zaidi.