COVID-19 yatawala mdahalo wa Harris na Pence
8 Oktoba 2020Katika mdahalo huo uliofanyika Jumatano usiku kwenye mji wa Salt Lake, Harris ameikosoa serikali ya Rais Donald Trump kwa kushindwa kulishughulikia janga la virusi vya corona. Harris, 55 amesema watu wa Marekani wameshuhudia kushindwa vibaya kwa serikali katika historia ya nchi hiyo.
''Na ukweli ni huu, watu 210,000 wamekufa kwenye nchi yetu katika miezi kadhaa tu iliyopita. Zaidi ya watu milioni 7 ambao wameambukizwa ugonjwa huu, mmoja katika watu watano biashara yake imefungwa. Tunawaangalia zaidi ya watu milioni 30 ambao wamejiandikisha kukosa ajira miezi kadhaa iliyopita. Januari 28, makamu wa rais na rais waliarifiwa kuhusu hali ya janga hili. Walijua na walikaa kimya,'' alisisitiza Harris.
Soma zaidi: Uhalisia wasambaratisha uongo wa Trump kuhusu corona
Kwa upande wake Pence, 61 amemkosoa Harris baada ya kuhoji iwapo chanjo ya corona iliyotangazwa chini ya utawala wa Trump kama inaweza kuaminiwa kutokana na shinikizo kali kwa rais kulidhibiti janga hilo. Pence amesema Trump amelipa kipaumbele suala la afya la Wamarekani.
''Taifa letu limepitia wakati mgumu sana mwaka huu. Lakini nataka kuwaambia watu wa Marekani kwamba, kuanzia siku ya kwanza kabisa, Rais Donald Trump ameweka mbele afya ya Wamarekani. Kabla ya kuwepo zaidi ya visa vitano Marekani, Rais Donald Trump alifanya kile ambacho hakuna rais mwengine yeyote wa Marekani aliyewahi kukifanya. Ndiyo maana alisitisha safari zote kutoka China, nchi ya pili kwa uchumi mkubwa duniani,'' alifafanua Pence.
Sera za kigeni zatajwa
Wagombea hao wenza pia wamezungumzia kuhusu sera za kigeni ambapo Pence ameunga mkono hatua ya Rais Trump dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS. Amesema jeshi la Marekani liliusambaratisha 'utawala wa ukhalifa' na kumuua kiongozi wa IS, Abu Bakr al-Baghdadi. Harris, amemshutumu Trump kwa kuwafukuza washirika wa Marekani na kuwakumbatia viongozi wanaotumia utawala wa kimabavu.
Rais Trump aliyekuwa anaufatilia mdahalo huo amezungumzia kuridhishwa na jinsi makamu wake alivyoshiriki. Katika ukurasa wake wa Twitter, Trump amesema Pence amefanya makubwa na amemkosoa Harris kwa kufanya makosa.
Naye mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democratic, Joe Biden, aliyekuwa akimtazama mgombea mwenza wake, amesema Harris ni mwerevu, ameonyesha kuwa mwenye uzoefu na amethibitisha kwamba ni mpiganaji wa watu wa tabaka la kati. Biden pia aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Sera za kiuchumi, ukosefu wa ajira, ongezeko la kodi, bima ya afya, mabadiliko ya tabia nchi pamoja na uhusiano kati ya Marekani na China, ni mada ambazo pia zimejadiliwa katika mdahalo huo uliofanyika kwa njia ya televisheni na kudumu kwa dakika 90. Mdahalo huo uliotawaliwa na utulivu, uliongozwa na mwandishi wa habari wa Marekani, Susan Page.
Wagombea hao wenza walitenganishwa na vizuizi vya vioo vilivyokuwa vimewekwa umbali wa futi 12 ambazo ni sawa na mita 3.7. Muda mchache kabla ya mdahalo huo, Harris na Pence walionyesha matokeo yao yanayothibitisha kwamba hawajaambukizwa virusi vya corona.
(AP, DPA, AFP, Reuters)