1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi akutana na mtangulizi wake na viongozi wa kidini

Saleh Mwanamilongo
22 Aprili 2020

Katika juhudi za kupambana na ugonjwa wa Corona nchini Congo, rais Felix Tshisekedi amekutana na mtangulizi wake Joseph Kabila na viongozi wa kidini .

Rais wa Congo Felix Tshisekedi (left) na mtangulizi wake Joseph Kabila watoa mwito wa mshikamano wa kitaifa katika kupambana na virusi vya Corona.
Rais wa Congo Felix Tshisekedi (left) na mtangulizi wake Joseph Kabila watoa mwito wa mshikamano wa kitaifa katika kupambana na virusi vya Corona.Picha: REUTERS

Katika juhudi za kupambana na ugonjwa wa Corona nchini Congo, rais Felix Tshisekedi amekutana na mtangulizi wake Joseph Kabila na viongozi wa kidini ambao amewaomba kujihusisha na kampeni ya kuwahamasisha wananchi kwa ajili ya kuepuka virusi vya Corona. Congo tayari imerikodi vifo 25 miongoni mwa watu 359 walioambukizwa kote nchini.

Katika taarifa iliyotolewa na ikulu mjini Kinshasa ni kwamba Tshisekedi na Kabila kwa muda wa masaa manne walizungumzia kuhusu athari za ugonjwa wa Corona kwenye sekta ya jamii na uchumi nchini Congo. Kwa pamoja wametoa mwito wa kuweko na mshikamano wa kitaifa kwa ajili a kupambana na ugonjwa huo. Hata hivyo mkutano huo umefanyika wakati ambapo tofauti zinadhihirika baina ya rais Tshisekedi na spika wa seneti Alexis Thambwe anayetokea vuguvugu la kisiasa la FCC la rais mstaafu Joseph Kabila.

Thambwe alielezea kwamba rais Tshisekedi alikiuka katiba kwa kutangaza hali ya dharura nchini bila idhini ya bunge. Korti ya katiba ilielezea kwamba hatua ya Tshisekedi haijakiuka katiba. Tayari baadhi ya wabunge kutoka vuguvugu la CACH linalomuunga mkono rais Tshisekedi, wameomba muendesha mashtaka mkuu amfungulie mashataka spika wa seneti kwa kile wanachoelezea kuwa ni kashfa dhidi ya rais Tshisekedi.

Wingu kwenye uhusiano baina ya FCC na CACH

Kwenye mitandao ya kijamii raia wa Congo wengi wamehoji ikiwa ni swala la Corona pekee ndilo viongozi hao wawili walilolizungumzia kwa mda wa masaa manne. Delphin Kapaya, mchambuzi wa masuala ya siasa nchini Congo amehisi kwamba mazungumzo hayo yanalenga kuzima moto baina ya vuguvugu ya FCC na CACH.

''Inaonekana kwamba kuna wingu baina ya FCC ya Kabila na CACH ya Tshisekedi.Kwa hiyo kutokana na tofauti za hivi karibuni,Tshisekedi ameamua kuzungumza moja kwa moja na Kabila kwa sababu yeye ndie kiongozi wa FCC ambako wametokea maspika wa bunge na seneti,lakini kila mtu amefanya maarifa yake na shabaa ya pande zote ni uchaguzi wa 2023''.

Picha: Getty Images/AFP/J.D. Kannah

Mapema rais Tshisekedi alikutana na viongozi wa kidini nchini ili kuwaomba mchango wao katika kupambana na ugonjwa wa Corona. Ujumbe huo wa viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali uliongozwa na kadinali wa kanisa katoliki jijini Kinshasa Fridolin Ambango, ambaye amesema waumini wanatakiwa kutekeleza marufuku ya ibada kama hatua mojawapo ya kupunguza maambukizi ya virusi vya corona.

''Adui wetu wa pamoja ni kirusi cha Corona, naomba tuweke mikakati ya pamoja ili kupambana na ugonjwa huo. Hivi sasa ibada ya pamoja ni marufuku kote nchini, lakini kila mtu anatakiwa kuliombea taifa mahala aliko, na tutaendelea kuwasiliana na waumini wetu kupitia mitandao na vifaa vya teknolojia ya kisasa.''

Hatua ya siku thelethini ya dharura iliyotangazwa na rais Tshisekedi itamalizika Ijumaa na bunge linatakiwa kukutana ili kuongeza muda huo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW