1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COVID: Je kirusi cha omicron ni hatari kiasi gani?

Stephanie Burnett, Fabian Schmidt, Esteban Pardo, John Juma2 Desemba 2021

Wanasayansi wameshauri watu kuchukua tahadhari lakini wasiingiwe na wasiwasi kuhusu aina ya kirusi cha corona omicron.

Symbolbild Corona Covid Variante Omicron B.1.1.529
Picha: DADO RUVIC/REUTERS

Swali linalosalia miongoni mwa wengi ni je kirusi hicho ni hatari kwa kiasi gani? DW inaangazia hatari zinazoweza kusababishwa na kirusi hicho kinachosambaa kwa kasi.

Watafiti wamebaini kwamba kirusi omicron kimejibadilisha mara 32 kwenye utandu wa protini pekee, kirusi hicho kinatumia utandu huo kupenya kwenye seli zetu na kutuambukiza.

Wataalamu wamesema kuna uwezekano kwamba kirusi hicho kipya kinaweza kukwepa kudhibitwa na kinga zetu za mwili kuliko aina nyingine za kirusi cha corona.

Soma: Uingereza yaidhinisha dawa ya kukabiliana na Omicron

Watafiti wanalenga nini kwenye uchunguzi?

Kutokana na hilo, watafiti wanachunguza aina tatu kati ya hizo mara 32 katika mfumo uitwao kitaalamu Furin cleavage site, kubaini kama kirusi kinaweza kugeuka kuwa ugonjwa mwilini.

Wataalamu wanasema ikiwa omicron inaweza kutuambukiza kwa urahisi na kugeuka kuwa ugonjwa, basi huenda kinaweza pia kusambaa kwa kasi na basi kasi ya maambukizi itakuwa juu.

WHO: Huenda kirusi cha Omicron kikasambaa kote duniani

Tumeshuhudia ongezeko la kasi ya maambukizi kwa sababu ya omicron katika baadhi ya maneneo ya kusini mwa Afrika. Lakini hiyo ni dhana tu. Utafiti ndio utathibitisha.

Watu wakisubiri kufanya vipimo vya virusi vya corona katika mji wa Duisburg Ujerumani 24.11.2021.Picha: Christoph Reichwein/imago images

Maswali Zaidi ni kuhusu madhara yake

Kwenye taarifa kwa shirika la Habari la DW siku ya Jumanne wiki hii, shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema haijafahamika wazi ikiwa maambukizi kutokana na omicron husababisha maumivu makali kuliko maambukizi kutokana na aina nyingine za kirusi cha corona ikiwemo delta.

"Data za awali zinadokeza kwamba kuna ongezeko la kasi ya maambukizi katika hospitali nchini Afrika Kusini. Lakini huenda hiyo ni kutokana na idadi jumla ya watu wanaoambukizwa na si kuwa wameambukizwa na omicron,” aliandika msemaji wa WHO.

Ujerumani, Uingereza na Italia zathibitisha visa vya Omicron

Pia haijulikani wazi lakini upo uwezekano kwamba huenda madaktari wakatafuta mbinu Zaidi za kuwatibu wale watakaougua Zaidi kutokana na omicron. Kwa mfano aina hiyo ya kirusi huenda kisidhibitiwe kwa kutumia dawa zinazotumiwa kudhibiti aina nyingine za kirusi cha corona.

Makali ya omicron ni ya kiwango gani?

Shirika la WHO limeliambia DW kwamba kwa sasa hakuna taarifa inayoeleza kwamba dalili zinazohusishwa na omicron ni tofauti na aina nyingine za kirusi cha corona. Lakini ufahamu kamili kuhusu makali ya kirusi hicho kwa mwanadamu utachukua siku au wiki kadhaa.

Aina mpya ya kirusi cha Covid-19 yapewa jina la Omicron

Ama kuhusu uimara wa chanjo zilizopo katika kudhibiti kirusi cha Omicron wanasayansi wanasema wanahitaji muda zaidi ndipo waweze kutoa majibu kamili kuhusu swali hilo.

Chanjo zilizopo ni madhubuti kiasi gani kudhibiti omicron?

Makampuni ya chanjo BioNTech-Pfizer, Moderna pamoja na Johnson & Johnson ni miongoni mwa makampuni yanayojaribu kutengeneza chanjo dhidi ya aina ya virusi vya omicron.Picha: Pavlo Gonchar/Zumapress/picture alliance

Afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya chanjo Moderna Stephane Bancel ametahadharisha kwamba huenda chanjo zilizopo kwa sasa zisiwe madhubuti kabisa dhidi ya omicron.

Lakini hakueleza zaidi ni kwa kiwango gani huku akisisitiza kwamba sharti watu wasubiri data kamili. Ameongeza kuwa kile ambacho wanayasanyi wametaja ni kwamba hali haitakuwa nzuri kutokana na omicron.

Mwanasayansi mkuu wa kampuni ya Pfizer Mikael Dolsten pia amesema kwenye mahojiano na jarida la kisayansi STAT kwamba kampuni yake inatumai chanjo ya ziada itaimarisha kinga dhidi ya omicron.

Makampuni ya chanjo BioNTech-Pfizer, Moderna pamoja na Johnson & Johnson ni miongoni mwa makampuni yanayojaribu kutengeneza chanjo dhidi ya aina ya virusi vya omicron.

Hadi Novemba 28, WHO ilisema hakukuwa na kifo chochote ambacho kilikuwa kimetokana na omicron.

Aina ya kirusi cha omicron kiligunduliwa mwanzo wiki ya pili ya mwezi Novemba.

Waandishi: Stephanie Burnett, Fabian Schmidt, Esteban Pardo

Tafsiri: John Juma

Mhariri: Chilumba Rashid

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW