1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utalii duniani kupata hasara ya zaidi ya dola trilioni 4

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
30 Juni 2021

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeeleza kwamba sekta ya utalii ulimwengu itakabiliwa na hasara kubwa kutokana na hatua za karantini pamoja na kukosekana kwa chanjo za COVID 19 katika nchi nyingi ulimwenguni.

Spanien Kanarische Inseln
Picha: Sarah Hucal/DW

Ripoti hiyo ya pamoja ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UNWTO) na la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) imesema kasi ndogo ya utoaji wa chanjo katika nchi zinazoendelea inachangia hasara hiyo wakati ambapo uchumi wa mataifa yanayoendelea unategemea sekta ya utalii. Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imekadiria hasara ya takriban dola trilioni nne.

Katibu Mkuu wa shirika la UNWTO, Zurab Pololikashvili amesema katika taarifa yake kuwa utalii ni njia ya kuleta mapato kwa mamilioni ya watu. Amesema kuendeleza kutoa chanjo kwa ajili ya kuzilinda jamii na kuwezesha kuanzishwa tena shughuli za utalii ni muhimu kwa sababu kutachochea fursa za kupatikana ajira na uzalishaji wa rasilimali zinazohitajika.

Jinsi janga la COVID lilivyoathiri usafiri

Ripoti hiyo imesema kusitishwa kwa safari ulimwenguni kote tangu mwanzo wa janga la corona kulisababisha hasara ya dola trilioni 2.4 katika sekta ya utalii na zile zinazohusiana na shughuli za utalii hapo mwaka jana. Hasara kama hiyo inaweza kutokea mwaka huu pia kulingana na kusuasua usambazaji wa chanjo.

Zuio la kusafiri lilisababisha kuongezeka kwa wastani wa asilimia 5.5 ya ukosefu wa ajira kwa watu wasio na ujuzi. Wakati huo huo wafanyikazi wa sekta ya utalii katika nchi ambazo hazina mfumo wa kuwalipa watu wasio na ajira wanatarajiwa kukosa kipato na hivyo kuwasababishia matatizo zaidi kutokana na kukosa fedha za kujikimu.

Nchi zinazoendelea zilikumbwa na upungufu mkubwa wa watalii mnamo 2020, kutoka asilimia 60 hadi 80. Maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni ya kaskazini mashariki mwa Asia, Asia ya Kusini, Oceania, Afrika Kaskazini na Asia ya kusini. Maeneo ya Amerika Kaskazini, Ulaya magharibi na Caribbean hayakuathirika sana.

Ugavi wa chanjo usio sawa umesababisha hasara

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imetahadharisha kwamba uchumi utaathirika zaidi katika nchi zilizo na viwango vya chini vya chanjo na kusababisha hasara katika pato jumla la mataifa hayo. Imesema baadhi ya nchi zimetoa chanjo chini ya asilimia 1 ya idadi ya watu wake huku zingine zikiwa zimefanikiwa kutoa chanjo kwa zaidi ya asilimia 60 ya watu wake.

Umoja wa Mataifa umesisitiza katika ripoti yake juu ya utoaji wa chanjo kwa wote ili ulimwengu uweze kuifufua sekta ya utalii na kukuza uchumi katika nchi mbalimbali duniani.

 Shirika la UNWTO limesema, utalii katika nchi za Ufaransa, Ujerumani, Marekani, Uingereza, na Uswizi unatarajiwa kufufuka na kuchipuka kwa haraka. Hata hivyo limesema halitarajii safari za kimataifa kurudi kwenye viwango vilivyokuwepo kabla ya kuzuka janga la corona mpaka mwaka ujao wa 2023.

Chanzo:/ https://p.dw.com/p/3vnjN

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW