1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CRAWFORD / Marekani:James Baker amaliza ziara yake ya ulaya na Asia, kwa kuahidiwa madeni ya Irak yatapunguzwa

30 Desemba 2003

Mjumbe maalu wa Rais wa Marekani kuhusu swali la madeni ya Irak kwa nchi za kigeni, Bwana james Baker, amemaliza ziara ya zaidi ya wiki moja, kuzishawishi nchi za Ulaya na Asia, kupunguza deni la Irak. Duru za serikali ya Marekani zimearifu Bwana james Baker, ambae ni Waziri wa zamani wa mambo ya kigeni, wakati wa utawala wa baba yake Rais wa sasa wa Marekani, leo alitarajiwa kusafiri hadi Crawford - Texas, ambapo Rais atakuwa katika kusherehekea siku kuu ya mwaka mpya, kumuarifu kuhusu matokeo ya ziara yake. Habari hizo zimesema kwa ujumla ziara hiyo ilikua ya mafanikio makubwa, kwa sababu baadhi ya nchi alikokwenda Bwana James Baker, zimekubali kimsingi kufuta sehemu kubwa ya madeni ya Irak kwa nchi hizo. Msemaji wa ikulu ya Marekani Trent Duffy, amesema hata hivyo kwamba mazungumzo yataendelea baina ya Marekani, nchi za Jumuia ya Umoja wa Ulaya na Japan, kuhusu viwango vya deni hilo vitakavyopunguzwa. Deni la Irak kwa nchi za kigeni, linakadiriwa kuwa zaidi ya biliyoni miamoja ishirini, dola za kimarekani. Wakuu wa Marekani wanasema deni hilo ni kikwazo kikubwa, kwa ujenzi mpya wa Irak.