Cristiano Ronaldo atunukiwa Ballon d'Or
14 Januari 2014Nadine Angerer akiibuka mchezaji bora mwanamke. Katika sherehe za kila mwaka za Ballon d'Or mjini Zurich, Shirikisho la Soka Ulimwenguni - FIFA lilimtaja Cristiano Ronaldo kama mchezaji bora ulimwenguni katika msimu wa mwaka wa 2012/2013. Mreno huyo alipigiwa kura na kumpiku nyota wa Barcelona Muargentina Lionel Messi na Mfaransa Frank Ribery wa Bayern Munich. Kama Messi angeshinda, tuzo hiyo ingekuwa yake ya tano mfululizo.
“Namshukuru kila mmoja, wachezaji wenzangu, timu ya taifa na familia yangu, kila mtu hapa” alisema Ronaldo aliyebubujikwa machozi.
“Sina maneno mengine ya kuielezea hali hii” aliongeza. CR7 alishinda tuzo hiyo ya FIFA ya mchezaji bora ulimwenguni mara ya mwisho katika mwaka wa 2008.
Mfaransa Franck Ribery alipigiwa upatu kushinda tuzo hiyo, kufuatia jukumu lake alilotekeleza katika klabu yake ya Bayern Munich, kushinda taji la Bundesliga, DFB Pokal na Champions League katika msimu wa 2012/2013. Pia alinyakua tuzo ya Shirikisho la Soka Ulaya – UEFA, mchezaji bora wa msimu wa 2012/2013.
Mshambuliaji wa Argentina Lionel Messi pia alikuwa kwenye orodha hiyo. Nyota huyo wa Barca alishinda mataji ya Ballon d'Or kwa miaka mitano mfululizo.
Ujerumani yashinda mataji matatu
Jupp Heynckes, kocha wa Bayern Munich katika msimu uliotangulia, alinyakua tuzo ya FIFA ya Kocha Bora wa Mwaka baada ya kuiongoza timu yake katika kutwaa mataji matatu.
Kocha mwenzake Mjerumani ambaye anaiongoza timu ya taifa ya wanawake Silvia Neid, alishinda tuzo hiyo kwa mara ya pili kwa upande wa wanawake. Aliishukuru FIFA kwa “kuitambua kandanda ya wanawake”.
Uwanjani katika soka la wanawake, mlinda lango wa Ujerumani na nahodha wa timu ya taifa Nadine Angerer, ambaye ni mchezaji bora wa mwaka barani Ulaya, alimpiku Mbrazil Marta na Abby Wambach wa timu ya taifa ya Marekani.
Mwandishi: Bruce Amani/DW/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Khelef