Cristiano Ronaldo mchezaji bora Ulaya
29 Agosti 2014Ronaldo mwenye umri wa miaka 29, alifunga penalti katika muda wa ziada wakati Real Madrid ikiizidi nguvu Atletico Madrid kwa ushindi wa magoli manne kwa moja katika fainali ya Champions League mwezi Mei. Alifunga jumla ya magoli 17 katika mechi 11 za Ulaya.
Kutokana na hali ya kutokuwa fit na pia uchovu wa kucheza mechi nyingi, CR7 alikuwa na wakati mgumu katika Kombe la Dunia nchini Brazil wakati Ureno wakibanduliwa nje ya hatua ya makundi. Laini mchezo wake katika jukwaa la Ulaya ulitosha kulishawishi jopo la wanahabari waliompigia kura.
Akizungumza mjini Monaco, CR7 alisema hangeweza kushinda taji hilo kibinafsi: “nina furaha kubwa sana. Ninasema ahsante kwa wachezaji wenzangu, familia yangu na marafiki zangu. Sina kombe hili katika jumba langu la makumbusho. Kakangu yuko hapa na atalipeleka huko moja kwa moja.”
Ni mara ya pili kwa Ronaldo kuchaguliwa mchezaji bora Ulaya baada ya kushinda taji la awali mwaka wa 2008 wakati akiichezea Manchester United.
Katika upande wa wanawake, mchezaji wa Ujerumani Nadine Kessler alishinda Tuzo ya Mchezaji Bora Mwanamke barani UIaya. Nahodha huyo wa Wolsfburg mwenye umri wa miaka 26 alishinda ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka jana akiwa na klabu hiyo, na pia taji la Ligi ya Wanawake ya Ujerumani.
Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Yusuf Saumu