Croatia na Ireland zajisafishia njia fainali za Euro
12 Novemba 2011Katika michuano ya soka iliyofanyika jana Ijumaa , timu za taifa za mataifa kadha zilikuwa zikipimana nguvu , ikiwa ni pamoja na michuano kuanzia ya kirafiki, ya kuwania kufuzu katika fainali za kombe la dunia na pia katika bara la Ulaya kulikuwa na michezo minne muhimu ya kuwania kufuzu kucheza fainali za kombe la mataifa ya ulaya mwakani. Timu nane ziliumana kuwania kujaza nafasi nne ambazo bado hazijajazwa katika orodha ya timu 16 zitakazowania taji la ubingwa wa mataifa ya Ulaya mwakani huko Ukraine na Poland. Ireland na Croatia jioni ya jana zimeondoa jinamizi linalowakumba kila mara kwa kuonyesha kandanda safi pamoja na kumimina mabao 7 wakati wakijihakikishia mkono mmoja ukiwa katika tikiti ya kufuzu kucheza katika fainali hizo. Katika mchezo huo wa kwanza ambapo mchezo wa pili utafanyika siku ya Jumanne, Jamhuri ya Czech iliisambaratisha Montenegro kwa mabao 2-0 mjini Prague.
Yaliyopita yamepita
Ireland ikihitaji kusahau yaliyopita katika mchezo kama huo wakati wakiwania kufuzu kucheza katika fainalia za kombe la dunia mwaka 2010 nchini Afrika ya kusini dhidi ya Ufaransa , ambapo tukio lililokuwa gumzo la watu wengi duniani la mshambuliaji wa Ufaransa Tierry Henry kuusukuma mpira kwa mkono na Gallas kutia bao, lilisababisha Ireland kukosa fainali hizo. Ireland jana ilijihakikishia nafasi ya kusonga mbele kwa kuichapa Estonia kwa mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza. Kwa upande wa Croatia ilikuwa ni ushindi wa furaha sana baada ya kuichapa Uturuki kwa mabao 3-0.
Matumaini yatoweka
Ni kwamba kila kitu kimekwisha amuliwa, kocha wa timu ya taifa ya Uturuki Guus Hiddink kutoka Uholanzi amesema. Ilikuwa ni vigumu mno kwetu baada ya Croatia kufunga bao la kuongoza katika dakika ya pili, nafikiri nitafanya mabadiliko kwa wachezaji ambao watacheza kwa ajili ya heshima tu ya Uturuki katika mchezo wa pili.
Ureno iliambulia sare ya bila kufungana na Bosnia Herzegovina na kuziweka timu hizo mbili katika nafasi ya kufa na kupona siku ya jumanne ambapo utakuwa mchezo wa kuamua mambo.
Ireland ikitaka kushiriki katika mashindano makubwa ya kwanza tangu mwaka 2002 iliposhiriki katika fainali za kombe la dunia, ilipata ushindi mjini Tallinn, kwa magoli ya Keith Andrews na Jon Walters, pamoja na magoli mawili ya Robbie Keane.
Katika mchezo wa kuwania kufuzu kucheza fainalia za kombe la dunia mwaka 2014, nchini Brazil, Argentina ilishindwa kushika usukani wa msimamo wa timu za America ya kusini, kwa kutoka sare ya bao 1-1 na Bolivia.Wabolivia wamepata point yao ya kwanza katika kampeni hiyo dhidi ya kikosi chenye nyota wengi cha Argentina ikiwa ni pamoja na Lionel Messi wa Barcelona pamoja na mchezaji wa kiungo wa PSG Javier Pastore.
Ujerumani ilikaribia kuonja kipigo
Kocha wa Ujerumani Joachim Loew amesisitiza kuwa timu yake itacheza vizuri katika mchezo wa kirafiki siku ya Jumanne dhidi ya makamu bingwa wa dunia Uholanzi baada ya Ujerumani kutolewa jasho na kuridhika na sare ya mabao 3-3 dhidi ya Ukraine mjini Kiev. Kikosi cha Loew kilinusurika kupata kipigo jana wakati kilipojitutumua kutoka kuwa chini kwa mabao 3-1 hadi mapumziko na kupata sare ya mabao 3-3 dhidi ya kikosi kitakachokuwa mwenyeji mwenza wa mashindano hayo ya fainali za euro 2012.
Nae Mario Balotelli na Giampaolo Pazzini waliufumania mlango wa Poland kila mmoja mara moja na kuipa ushindi Italia wa mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji hao wenza wa kombe la mataifa ya Ulaya zitakazofanyika nchini Poland na Ukraine mwakani.
Uganda nao wamo
Na katika bara la Afrika Cameroon iliishinda Sudan kwa mabao 3-1, wakati Senegal iliibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Guinea nayo Morocco ikaangukia pua mbele ya Uganda kwa kuchapwa bao 1-0, na Burkina Faso ilitoka sare na Mali kwa kufungana bao 1-1.
Jioni ya leo Afrika kusini itaonyeshana kazi na Ivory Coast, wakati Tunisia na Algeria zitapimana ubavu mjini Algiers, na Botswana na Nigeria zina miadi mjini Benin na kesho Jumapili Morocco itakuwa na kibarua dhidi ya Cameroon, wakati Sudan na Uganda zitatambua nani zaidi kati yao mjini Marrakech.