1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Croatia yawabandua nje Cameroon

19 Juni 2014

Mario Mandzukic alifunga magoli mawili katika mchezo wake wa kwanza wa Kombe la Dunia wakati Croatia ikiwabamiza Cameroon magoli manne kwa sifuri na kuwabandua nje ya tamasha hilo.

WM 2014 Gruppe A 2. Spieltag Kamerun Kroatien
Picha: Reuters

Matokeo hayo sasa yamehakikisha kuwa kutakuwa na mchuano wa kusisimua katika duru ijayo kati ya Croatia na Mexico, huku Croatia ikihitaji ushindi ili kusonga mbele kutoka awamu ya makundi, nayo Mexico ikihitaji tu sare.

Huku ikionyesha bidii, ujuzi na mashambulizi makali, Croatia huenda ingefunga hata magoli mengi zaidi kuliko yale yaliyopachikwa wavuni na wachezaji Ivana Olic, Ivan Pericic na Mario Mandzukic, lakini walipoteza nafasi chungu nzima za wazi mbele ya lango la Cameroon.

The Indomitable Lions, ambao walicheza bila ya mshindi wa zamani wa Tuzo ya mchezaji bora wa mwaka, Samuel Eto'o aliyepata jeraha la goti, waliuanza mpambano huo kwa kasi na walionekana kuitishia safu ya ulinzi ya Croatia.

Lakini kiungo Alex Song aliwaharibia wenzake hata zaidi baada ya kumpiga kumbo Mario Mandzukic mgongoni katika dakika ya 40 na hapo akaonyeshwa kadi nyekundu na refarii.

Licha ya Croatia kuwa kifua mbele, mechi hiyo ilikuwa ikienda kila upande hadi wakati Song alipoonyesha uwendawazimu wake. Lakini katika kipindi cha pili, mchezo uliegemea upande mmoja katika lango la Cameroon, huku Croatia wakikosa nafasi kadhaa za wazi kutokana na pasi zao nzuri na wingi wa wachezaji uwanjani. Cameroon walijaribu kubisha katika lango la Croatia wakati mshambuliaji Eric Choupo Moting alipovurumisha kombora hadi juu ya lango.

Mwandishi: Bruce Amani/dpa
Mhariri: Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW