Croatia yawapeleka wahamiaji Hungary
19 Septemba 2015Hatua hiyo inakuja wakati nchi kadhaa katika eneo la Balkan zimefunga mipaka yake, zikizuwia njia muhimu kuingia katika mataifa ya magharibi na kuwaacha maelfu wakiwa wamekwama.
Na wakati Croatia imesema imefikia kiwango cha kupita kiasi cha wakimbizi baada ya zaidi ya wahamiaji 14,000 kuwasili katika masaa 48 yaliyopita, imeanza kuwaruhusu wahamiaji hao kuelekea mpaka wa kaskazini mashariki na Hungary, nchi iliyoko katika eneo linaloingilia wakimbizi , imeapa kulinda mipaka yake dhidi ya wimbi la wakimbizi.
Saa chache kabla , Budapest ilianza kujenga uzio mpya wa waya kuwazuwia wahamiaji katika mpaka wake na Croatia, na kuanzisha mpambano mwingine wa kidiplomasia wakati Hungary inaishutumu Croatia kwa kuwasukuma wakimbizi kuvunja sheria kwa kuwapeleka katika mpaka na Hungary.
Tarakimu mpya
Kukiwa hakuna ishara ya kupungua kwa watu hawa wenye shida wanaotafuta hifadhi katika mataifa ya Ulaya, tarakimu mpya zinaonesha Umoja wa Ulaya umepokea karibu robo ya waombaji hifadhi milioni moja katika miezi mitatu hadi Juni mwaka huu.
Na wakati mwili wa mtoto mwingine ukielea katika ufukwe wa pwani ya Uturuki, tarakimu mpya kutoka shirika la kimataifa la kuwahudumia wahamiaji (IMO) zinaonesha kwamba karibu watu 474,000 hadi sasa mwaka huu wameweza kukabili safari za hatari kuvuka bahari ya Mediterania kufika Ulaya.
Baada ya Hungary taifa lililoko katika eneo linaloingilia wakimbizi katika Umoja wa Ulaya kufunga mpaka wake wa kusini na Serbia mapema wiki hii, maelfu ya wahamiaji na wakimbizi wakielekea katika mataifa ya magharibi, walitafuta kufungua njia mpya kuelekea magharibi kupitia Croatia na Slovenia na kuingia Austria.
Imeelemewa na mzigo
Lakini baada ya siku mbili za kuwaruhusu watu kuingia, Croatia jana Ijumaa,nchi hiyo ilisema imefikia hali ya kuelemewa na mzigo huo, na kufunga vivuko saba vya kuingilia nchini humo katika mpaka wake wa mashariki na Serbia.
"Kuanzia leo tutaanza kutumia mipango mipya ," Waziri mkuu wa Croatia Zoran Milanovic amesema wakati Zagreb ikianza kuyaruhusu mabasi kadhaa kuelekea mpakani. "Tuna uchaguzi gani tena?"
"Hungary imefunga mipaka yake kwa waya wa seng'enge, hilo sio suluhisho, lakini watu hawa kubaki nchini Croatia sio suluhisho pia."
Mwandishi wa shirika la habari la afp katika kijiji kilichoko katika mpaka wa Hungary cha Beremend amehesabu mabasi 22 , kila moja likiwabeba karibu watu 60 yakiwasili katika upande wa Croatia ambako walipokewa na kiasi ya polisi 250 wa Hungary na wanajeshi.
Mabasi mawili kati ya hayo yaliruhusiwa kuvuka, wakati abiria wake wakiruhusiwa kushuka na kuingia katika mabasi ya Hungary ambayo yaliondoka kuelekea mahali pasipojulikana, amesema.
Huduma za magari ya kuwasafirisha wahamiaji kutoka Tovarnik katika mpaka wake wa mashariki na Serbia na mji wa Beli Manastir , ulioko karibu na mpaka na Hungary, ambako polisi wengi wamewekwa mitaani , karibu mabasi 10 yaliyo matupu yamesimama yakisubiri.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Yusra Buwayhid